Mwimbaji wa Marekani, Mariah Carey, 56, ameibuka tena na ushindi katika kesi ya hakimiliki iliyohusu wimbo wake wa Krismasi, All I Want For Christmas Is You (1994) ambao huchezwa sana duniani msimu huu wa sikukuu.

Hiyo ni baada ya jaji kuamuru waliomshtaki walipe faini (sanctions) ya Dola 92,000 wastani wa Sh226.5 milioni. Uamuzi huo huwenda ukaongeza furaha kwa staa huyo hasa katika msimu huu ambao wimbo humrejesha katika chati.

Kwa mujibu wa nyaraka mpya za kisheria zilizopatikana na TMZ, jaji aliyesikiliza kesi hiyo alibaini kuwa madai yaliyofunguliwa dhidi ya Mariah Carey hayakuwa na msingi wa kisheria.

Jaji alieleza kuwa kesi hiyo ilikosa ushahidi wa kutosha na ikaonekana kuwa ni jaribio la kufungua shauri lisilo na mashiko, jambo lililomlazimu kuchukua hatua kali ili kuzuia tabia hiyo kuendelea katika mfumo wa sheria.

Kutokana na uamuzi huo, Mariah Carey alipatiwa Dola 92,000 kama faini inayotakiwa kulipwa na walioshtaki, ikiwa ni pamoja na kumlipa kufidia ya gharama za kisheria na usumbufu alioupata.

Aidha, jaji aliamuru fedha zaidi zilipewa na wahusika wengine waliokuwa wamehusika katika kesi hiyo. Kwa jumla, kiasi cha fedha kinachotakiwa kulipwa kinafikia takribani Dola 110,000.

Ikumbukwe kesi hiyo ilianza Novemba 2023, pale wanamuziki Andy Stone na Troy Powers walipomfungulia Mariah Carey kesi wakidai kuwa aliiga wimbo wao wa mwaka 1989 uliokuwa na jina lilelile (All I Want For Christmas Is You).

Wawili hao walidai kuwa wimbo wa Mariah Carey uliiba muundo, maneno na wazo kuu la kazi yao ya awali.

Katika madai yao, Stone na Powers walikuwa wakitaka fidia ya angalau Dola20 milioni, wakidai kuwa Mariah Carey alijinufaisha kibiashara kwa kutumia kazi yao bila ruhusa.

Hata hivyo, baada ya mahakama kuchambua nyaraka, ushahidi wa kitaalamu wa muziki na hoja za pande zote, jaji alitupilia mbali kesi hiyo mnamo Machi 2024, akisema hakukuwa na ushahidi unaothibitisha kuwa Mariah alinakili wimbo huo.

Hatua ya jaji kuamuru walioshtaki pamoja na mawakili wao kulipa faini imeonekana kama onyo kali kwa watu wanaofungua kesi zisizo na msingi wa kisheria, hususani katika masuala ya hakimiliki ya muziki.

Ikumbukwe wimbo huo ulirekodiwa Agosti 1994 katika studio za The Hit huko New York na kuwekwa katika albamu yake ya nne na albamu ya kwanza ya sikukuu, Merry Christmas (1994).

All I Want For Christmas Is You, ni wimbo uliandikwa na kutayarishwa na Mariah Carey na Walter Afanasieff, na ulitolewa kama wimbo wa kwanza katika albamu hiyo iliyotoka rasmi Oktoba 29, 1994.

Kufuatia mafanikio ya albamu yake, Music Box (1993), Mariah Carey na Columbia Records na aliyekuwa mumewe, Tommy Mottola, Mkuu wa Columbia Sony Music Entertainment, walianza kupanga miradi mikubwa ndipo likaja wazo la kufanya albamu ya Krismasi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *