Huku hali ikiendelea kutulia huko Caracas, Wavenezuela wanazungumzia taarifa za kukamatwa kwa Rais Nicolás Maduro na Marekani kwa matumaini, hofu, na kutokuwa na uhakika.

Watu walianza kujitokeza mitaani Jumamosi baada ya usiku uliokumbwa na milipuko katika eneo la Bonde la Caracas, huku hisia zikiwa tofauti kuanzia wanaosherehekea hadi wenye kushutumu.

Dina, mkazi wa eneo hilo, aliambia BBC kwamba kwa sasa, anaishukuru Marekani kwa “kumuondoa Maduro madarakani” kwa sababu sasa, “angalau anaweza kuona tena matumaini”.

Hata hivyo, hali ya kisiasa bado ni ya kusuasua, sehemu ya sababu hakusema jina lake halisi kwa BBC.

Jorge, Mvenezuela mwingine anayeishi karibu na Caracas, aliambia BBC kwamba ingawa anashukuru “kuungwa mkono na Trump na Marekani nzima”, anahofia siku zijazo hazitakuwa rahisi.

“Sasa kwa kuwa wanamchukua Maduro, nini kitatokea” Jorge aliambia BBC. “Hatuna uhakikisho wa chochote. Hivyo kuna hali ya kutokuwa na uhakika. Hatujui siku zijazo mambo yatakuwa namna gani.”

Wafuasi wa serikali ya Maduro pia wamekuwa wakikusanyika katika mitaa ya Caracas, wakitaka Marekani imwachilie kiongozi wao. Meya wa Caracas Carmen Meléndez, mfuasi imara wa serikali, alijiunga na mkutano huo kupinga kile alichokiita Maduro “utekakwa nyara”.

Mapema Jumamosi, vikosi vya Marekani chini ya Rais Donald Trump vilitekeleza mfululizo wa mashambulizi yaliyolenga mji mkuu wa Venezuela, na hatimaye kumkamata kiongozi huyo wa nchi hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *