Polisi wa Nigeria wameripoti kuwa watu wasiopungua 50 wameuawa katika shambulio lililofanywa na magaidi wenye silaha katika soko la kijiji katika Wilaya ya Kabe, eneo la Serikali ya Mtaa ya Borgu katika Jimbo la Niger.

Uongozi wa polisi katika jimbo la Niger umearifu kuwa magaidi hao juzi Jumamosi walishambulia soko la Kasuwan Daji katika kijiji cha Demo na kulichomota moto, kuiba bidhaa na kuwateka nyara raia kadhaa. 

Wasiu Abiodun, Msemaji wa Polisi katika jimbo la Niger amesema kuwa Januari tatu majira ya mchana walipokea taarifa kwamba majambazi kutoka msitu wa Hifadhi ya Taifa unaopatikana na wilaya ya Kabe walivamia eneo la Kasuwan Daji katika kijiji cha Demo na kulichoma moto soko hilo, kuiba katika maduka mbalimbali na kuondoka na vyakula. 

Msemaji huyo wa polisi katika jimbo la Niger, ameongeza kusema kuwa, timu ya usalama imetembelea eneo la tukio na kuthibitisha kuwa watu wasiopungua 50 wameuawa katika hujuma hiyo ya kigaidi. 

“Baadhi ya watu walitekwa nyara. Juhudi zinaendelea kufanywa ili kuwakomboa wahanga,” amesema Abiodun.

Katika wiki za karibuni jimbo la Niger limeshuhudia mashambulizi ya kigaidi yanayojirudia hasa katika jamii za vijijini zilizo katika hatari ya kushambuliwa na makundi yenye silaha yanayotekeleza hujuma kutokea katika maeneo misituni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *