
Rais Gustavo Petro wa Colombia ametahadharisha kuwa nchi za Amerika ya Latini ni lazima ziungane, kinyume chake zitakabiliwa na hatari ya kufanywa kama watumwa. Rais wa Colombia ametamka haya kufuatia vitisho mtawalia vya Rais Donald Trump wa Marekani vinavyojumuisha uwezekano wa kufanyika oparesheni ya kijeshi dhidi ya Colombia.
Gustavo Petro amesema haya baada ya Trump kumtishia wakati alipozungumza na waandishi wa habari jana akiwa ndani ya ndege ya Air Force One, siku moja baada ya jeshi la Marekani kumteka nyara Rais Nicolas Maduro wa Venezuela na mke wake, Cilia Flores kufuatia hujuma ya kijeshi ya Washington dhidi katika mji mkuu wa Venezuela, Caracas.
Akiwa ndani ya ndege, Trump ameda kuwa Colombia na Venezuela ni nchi zenye matatizo sana na amemtuhumu Rais Petro kuwa anaongoza serikali inayohusika katika uzalishaji wa kokeini na usafirishaji haramu wa dawa za kulevya kuelekea Marekani. Rais wa Marekani amesema Rais wa Colombia hatafanya hivyo kwa muda mrefu.
Alipoulizwa iwapo matamashi yake hayo yalikuwa yakiashiria uwezekano wa kutekelezwa mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Colombia, Trump alijibu; “Inasikika vizuri kwangu.”
Rais Gustavo Petro wa Colombia amejibu vitisho hivyo vya Trump kwa kutoa wito kwa mataifa ya Amerika Kusini kuwa bega kwa bega. “Marekani ndiyo nchi ya kwanza duniani kulipua mji mkuu wa nchi ya Amerika Kusini katika historia yote ya binadamu,” ameandika Rais wa Colomia katika chapisho alilotuma katika ukurasa wake wa mtandao wa X akimaanisha shambulio dhidi ya mji mkuu wa Venezuela, Caracas.
Rais wa Colombia amesema kuwa mataifa ya Amerika Kusini yanapaswa kuungana ili kuwa ukanda wenye uwezo wa kushirikiana na ulimwengu kwa masharti yao, kufanya biashara na kushirikiana kimataifa badala ya kutegema “kaskazini pekee.”