Mkuu wa Mkoa wa Lindi,Zainab Telack,amekuta na na wawekezaji wa kiwanda cha kusindika na kuchakata malighafi ya vifuu vya nazi kinachomilikiwa na kampuni ya African Coconut Material Production, ambacho ujenzi wake unaendelea katika Kijiji cha Mtange, Manispaa ya Lindi.

Telack amesema kuwa Mkoa wa Lindi uko tayari kuendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wote, akiwahimiza wasisite kuja kuwekeza katika mkoa huo.

Ameeleza kuwa milango ya uwekezaji ipo wazi, na kwamba Serikali ya Mkoa itaendelea kutoa ushirikiano thabiti na wa karibu kwa wawekezaji ili kuboresha mazingira ya uwekezaji, kuchochea ukuaji wa uchumi, na kuinua maisha ya wananchi wa Mkoa wa Lindi.

Aidha kwa upande wa Wawekezaji wameishukuru Serikali ya Mkoa wa Lindi kwa ushirikiano mzuri wanaoendelea kupewa, wakieleza kuwa ujenzi wa kiwanda umefikia hatua nzuri.

Pia wameahidi kuhamasisha wawekezaji wengine kuja kuwekeza katika mkoa huo kutokana na mazingira mazuri ya uwekezaji, ushirikiano mzuri kati ya serikali na sekta binafsi, pamoja na hali ya amani iliyopo.

Akizungumza kwa niaba ya kampuni hiyo, mkalimani wao Ndugu Katoro Chikula amesema kuwa kampuni inatarajia kuanza kukusanya vifuu vya nazi kuanzia Januari 7, 2025, ambapo bei ya tani moja ya vifuu imekadiriwa kuwa Shilingi 200,000/=.

Wananchi na wakulima wa Mkoa wa Lindi wanatarajiwa kunufaika kwa kiasi kikubwa na uwekezaji huo, kwani utaongeza ajira kwa wananchi pamoja na kuwawezesha wakulima wa zao la nazi kupata kipato kupitia uuzaji wa vifuu vyao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *