
Serikali ya Somalia Jumanne imelaani ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Gideon Saar, katika Somaliland, ikieleza kuwa ni “uvunjaji wa mamlaka usioidhinishwa” na ikaitaka Tel Aviv kusitisha mara moja hatua zote zinazodhoofisha uhuru na umoja wa ardhi ya Somalia.
Katika taarifa rasmi, Wizara ya Mambo ya Nje ya Somalia imesema kuwa ziara hiyo ni “kuingilia mambo ya ndani na hivyo ni jambo lisilokubalika” katika masuala ya taifa huru mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Somalia imeongeza kuwa hatua hiyo inakiuka Hati ya Umoja wa Mataifa, Hati ya Umoja wa Afrika, na kanuni zilizowekwa za uhusiano wa kimataifa, ikiwemo usawa wa mamlaka, heshima ya mipaka na kutokuingilia mambo ya ndani.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa Somaliland ni sehemu “kamili na isiyotenganishwa” ya Somalia, na kwamba uwepo wowote rasmi, mawasiliano au ushirikiano katika ardhi ya Somalia bila idhini ya serikali ya shirikisho ni haramu, batili na hauna athari yoyote ya kisheria.
Somalia imezitaka taasisi za kimataifa ikiwemo Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), pamoja na washirika wengine wa kimataifa, kuthibitisha tena kwa maneno wazi na yasiyoacha shaka msimamo wao wa kuunga mkono uhuru na mipaka inayotambulika kimataifa ya Somalia.
Ziara ya Saar imefanyika takribani wiki mbili baada ya utawala haramu wa Israel kutangaza kutambua rasmi Somaliland kama taifa huru, hatua iliyosababisha ghadhabu kubwa kimataifa. Mnamo Desemba 26, Israel ilitangaza kutambua Somaliland, na kuwa nchi pekee duniani kufanya hivyo. Hatua hiyo imepingwa vikali na mataifa ya Afrika na Kiarabu, yakieleza kuwa ni haramu na tishio kwa amani na usalama wa kimataifa.
Somalia imesisitiza tena msimamo wake thabiti na usioweza kujadiliwa kuhusu uhuru, umoja wa kitaifa na heshima ya mipaka yake, ikikataa vikali hatua ya Israel.
Tangu kutangaza kujitenga mwaka 1991, Somaliland imekuwa ikijitawala kama kitengo cha kiutawala, kisiasa na kiusalama, bila kutambuliwa rasmi kimataifa.