
Waziri wa Ulinzi wa Pakistani amemtaja Waziri Mkuu wa Israel kuwa mtenda jinai anayechukiwa zaidi katika historia na kusema: “Uongo wa Benjamin Netanyahu dhidi ya miradi ya nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayoendeshwa kwa malengo ya amani ulikuwa kisingizio tu cha kuhalalisha mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran.
Katika mahojiano na mtandao wa habari wa Geo mjini Islamabad, Khawaja Muhammad Asif amekosoa mwenendo wa uchokozi wa Rais wa Marekani, Donald Trump dhidi ya Venezuela.
Ameongeza kuwa: “Hatua yoyote ya uvamizi wa Marekani dhidi ya jirani yetu Iran itakuwa changamoto pia kwa Pakistan.”
Waziri wa Ulinzi wa Pakistani amemhutubu Trump kwa kusema: “Ikiwa Rais wa Marekani anajali kwa dhati ubinadamu, basi anapasa kumtia nguvuni Netanyahu, mshtakiwa mtoro na mtenda jinai mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia na kumfungulia mashtaka katika mahakama za Marekani.”
Waziri wa Ulinzi wa Pakistan ameashiria uropokaji wa Waziri Mkuu wa Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika muongo mmoja uliopita na kusema: Netanyahu amekuwa akidanganya na kutoa madai yasiyo na msingi kuhusu miradi ya nyuklia ya Iran tangu mwaka 2012; na amekuwa akidai kuwa Iran inakaribia kutengeneza bomu la nyuklia katika hali ambayo madai hayo ya uwongo yalikuwa ni kisingizio tu cha Israel ili kuhalalisha chokochoko zao dhidi ya Iran katika siku zijazo.