Ikulu ya White House ya Marekani imesema Rais Donald Trump wa nchi hiyo na washauri wake wanatathmini “machaguo mbali mbali” katika jitihada za kulitwaa eneo la Greenland, likiwemo chaguo la kutumia jeshi la nchi hiyo.

“Rais Trump ameeleza wazi kwamba, kuichukua Greenland ni kipaumbele cha usalama wa taifa kwa Marekani, na ni muhimu katika kuwazuia maadui zetu katika eneo la Arctic,” Katibu wa Vyombo vya Habari wa White House, Karoline Leavitt amesema katika taarifa.

“Rais na timu yake wanachunguza machaguo kadhaa ili kutekeleza lengo hili muhimu la sera ya kigeni. Na bila shaka, kutumia jeshi la Marekani daima ni chaguo kwa kamanda mkuu,” ameongeza Leavitt, licha ya kisiwa hicho tayari kuwa na kambi ya kijeshi ya Marekani.

Kauli hiyo ya Marekani kutaka kutumia nguvu za kijeshi kuitwaa Greenland inakuja baada ya Trump kudai siku Jumatatu kwamba, kutwaliwa Greenland kunakaribia, akisisitiza kuwa anataka (kumiliki) eneo la Arctic “sasa hivi.”

Waziri Mkuu wa Denmark amepinga madai mapya ya Trump kuhusu kulimiliki eneo la Greenland na kuitaka Washington ikome kutoa vitisho dhidi ya mshirika wake huyo, akiyataja matamshi hayo ya Trump kuhusu Greenland kuwa ya kipuuzi kabisa.

Matamshi ya Trump tayari yameibua hofu nchini Denmark, ambayo inahusika na ulinzi wa Greenland, hasa kutokana na uvamizi wa kijeshi wa hivi karibuni wa Washington dhidi ya Venezuela, ikiwa ni pamoja na kutekwa nyara kwa Rais Nicolas Maduro na mkewe, Cilia Flores.

Katika kujibu, viongozi wa Ufaransa, Ujerumani, Uingereza na nchi nyingine kadhaa waliungana na Waziri Mkuu wa Denmark, Mette Frederiksen, Jumanne kuitaka Washington kuheshimu uhuru wa Denmark, wakisisitiza kwamba usalama wa Arctic ni kipaumbele muhimu kwa NATO, ambayo inajumuisha Marekani na Greenland.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *