Katika tarifa yake ya pamoja kutoka Geneva Uswisi na Port Sudan nchini Sudan, tangu kuzuka kwa mapigano Aprili 15, 2023, zaidi ya watu milioni 15 wamelazimika kuyahama makazi yao ndani ya Sudan na kuvuka mipaka kwenda nchi jirani, hali iliyoifanya Sudan kuwa na janga kubwa zaidi la uhamiaji wa ndani duniani kwa sasa.
Msafara wa magari ya Umoja wa Mataifa ukielekea El Geneina huko Darfur Magharibi, Sudan. (Maktaba)
“Siku elfu moja za migogoro zimewaathiri vibaya watu wa Sudan,” amesema Amy Pope, Mkurugenzi Mkuu wa IOM katika taarifa hiyo na kuongeza kuwa “Nyuma ya kila takwimu za watu waliokimbia makazi yao kuna familia inayofanya kila iwezalo kuwalinda watoto wao, kuhifadhi heshima yao na kuishi bila chochote. Ujasiri wa watu wa Sudan lazima ukumbane na hatua endelevu za kimataifa – hatua inayowalinda raia, inayounga mkono familia zilizokimbia makazi yao, na kuunda mazingira ya amani ili watu waweze kurudi salama, kupona na kujenga upya maisha yao.”
Vita na majanga
Kwa mujibu wa IOM, matukio 743 yamesababisha uhamaji kote nchini, yakiwemo matukio 524 yanayohusiana na vita pamoja na majanga ya asili kama mafuriko na moto. Katika kilele cha mgogoro huo, takribani asilimia 15 ya wakimbizi wa ndani duniani walikuwa kutoka Sudan, sawa na mtu mmoja kati ya saba wa wakimbizi wa ndani duniani.
Hata kabla ya vita vya sasa, Sudan tayari ilikuwa na watu milioni 3.8 waliokimbia makazi yao. Tangu mwezi Aprili 2023, asilimia 41 yao wamelazimika kuhama tena.
Moja tu ya majengo mengi katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum, yaliyoathiriwa na vita vilivyozuka kati ya Vikosi vya Wanajeshi vya Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka vya kijeshi mnamo Aprili 2023.
Ingawa baadhi ya wananchi wameanza kurejea nyumbani, hali ya usalama, miundombinu na huduma muhimu bado ni dhaifu.
Watoto wanaendelea kubeba mzigo mkubwa wa mgogoro huu, wakichangia asilimia 55 ya wakimbizi wa ndani, na wengi wao wakikabiliwa na hatari za ulinzi, kukosa elimu na mustakabali usio na uhakika.