
Kwa mujibu wa Mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu milioni 30 wanahitaji msaada wa kibinadamu nchini Sudan, idadi hiyo ikijumisha watoto zaidi ya milioni 15 wanaohitaji msaada wa dharura ili kuendelea kuishi. Aidha zaidi ya watu milioni 9.8 wamelazimika kuyahama makazi yao, hali inayozidisha changamoto za chakula, maji, afya na elimu.
Katika kipindi cha siku 1000 za vita hivi, Umoja wa Mataifa pamoja na mashirika yake umeendelea kutoa misaada ya kuokoa maisha, licha ya changamoto za kiusalama na upatikanaji wa maeneo yenye uhitaji mkubwa.
Leo, tunaangazia kwa undani mchango wa Shirika la Umoja wa Mataifa la linalohusika na kuhudumia watoto UNICEF.
UNICEF imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia watoto na familia zilizoathiriwa na vita.
Kupitia miradi ya maji, usafi na afya, shirika hilo limefanikiwa kuwafikia zaidi ya watu milioni 12.6 kwa huduma ya maji salama, ikiwa ni zaidi ya lengo la mwaka, hatua iliyosaidia kudhibiti magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu katika maeneo ya wakimbizi na yaliyokumbwa na mapigano.
Katika sekta ya lishe, hali ni mbaya zaidi. UNICEF na washirika wake wamewapatia matibabu ya utapiamlo mkali watoto takriban 600,000 wenye umri wa chini ya miaka mitano mwaka 2025, huku njaa kali ikithibitishwa katika baadhi ya maeneo kama Al Fasher na Kadugli
Elimu nayo imeathirika pakubwa kutokana na shule nyingi kufungwa au kutumiwa kama makazi ya wakimbizi. Hata hivyo, UNICEF imeanzisha maeneo salama ya kujifunzia na kusambaza vifaa vya shule kwa mamia ya maelfu ya watoto, ili kuhakikisha wanaendelea kupata elimu hata katikati ya vita.
Licha ya mafanikio haya, UNICEF inaonya kuwa msaada wake nchini Sudan unakabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha. Kwa mwaka 2025, UNICEF imetoa ombi la dola milioni 950 ili kukidhi mahitaji ya dharura ya watoto na familia zao. Hata hivyo, zaidi ya asilimia 51 ya fedha hizo bado hazijapatikana, hali inayohatarisha kuendelea kwa huduma muhimu za kuokoa maisha
Leo ikiwa ni siku 1000 tangu vita kuanza nchini Sudan, ujumbe wa Umoja wa Mataifa na UNICEF unabaki kuwa mmoja: kuna haja ya dharura ya kuongeza ufadhili, kulinda raia, na kuhakikisha watoto wa Sudan hawapotezi haki yao ya kuishi, kujifunza na kuwa na maisha yenye heshima.