Wanawake hao wameungana chini ya kikundi cha wanawake cha Paran, ambacho kinatekeleza miradi ya upandaji miti, matumizi ya tiba asilia na kilimo endelevu kama njia ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha ustawi wa jamii.
Wanawake huko Narok, Kenya, hupanda miche ya miti kwa ajili ya kuhifadhi misitu.
Kwa wanawake wa Kikundi cha Orumokonge, upandaji wa miti si tu juhudi ya uhifadhi wa mazingira bali pia chanzo cha kipato cha kusaidia familia. Mwenyekiti wa kikundi hicho, Kirotiana Kipsa, anaeleza jinsi miti inavyobadilisha maisha yao.
“Tunafurahia kupanda miti kwa sababu inaboresha mazingira yetu. Pia, tunapouza miti, tunaweza kupata ada ya shule kwa watoto wetu.”
Mbali na mchango wake kwa mazingira, miti imeendelea kuwa chanzo muhimu cha tiba asilia kwa familia nyingi. Noonkowa Koini anaeleza kuwa maarifa ya jadi yanatumika kulinda afya.
“Hapa tunapanda miti, ambayo ina faida nyingi kwetu. Baadhi ya miti hii ni ya dawa. Tunazitumia kutengeneza tiba kwa watoto wetu wanapopata mafua, na kwa wanawake, tunazitumia kutibu maumivu ya tumbo, mgongo na magonjwa mengine. Miti hii inatusaidia sana.”
Kupitia mafunzo yaliyotolewa na Paran, wanawake wameongeza kilimo cham boga za majani na hivyo kuwa na uhakika wa chakula nyumbani. Leah Ndieeti anafunguka.
“Paran walipotembelea kikundi chetu, walitufundisha jinsi ya kulima mboga kwa ufanisi zaidi. Mafunzo hayo yametuwezesha kuzipatia familia zetu mahitaji bila kukopa kwa majirani. Huu ni maendeleo mazuri kwetu. Waume na watoto wetu wanafurahi, na sasa ni rahisi kupata mboga moja kwa moja kutoka bustanini. Tunashukuru sana.”
Kituo cha rasilimali cha Wanawake cha Paran huko Narok, Kenya, kukuza uhifadhi wa misitu na maendeleo ya jamii.
Lakini kubwa zaidi ni wanawake kuweza kujitegemea kama asemavyo Elizabeth Murero.
“Tuna shukrani kwa sababu sasa tuna shughuli endelevu. Tunajishughulisha na kazi zetu na tunajiajiri. Tumekuwa huru zaidi na tunajitegemea. Tunawashukuru mama Lucy na mama Betty kwa kutuongoza. Asanteni sana, na Mungu awabariki.
Pamoja na faida bado kuna changamoto.
“Hata hivyo, changamoto yetu kubwa bado ni upatikanaji wa maji. Kwa sasa tunafurahi kwa sababu mvua inanyesha, lakini mvua ikikosekana tunapata shida sana. Hulazimika kutembea umbali mrefu kuchota maji mtoni. Tumechimba visima lakini hukauka haraka. Mto uko takribani kilomita 20 kutoka hapa, na safari ya kwenda na kurudi huchukua karibu saa tatu.”