Dar es Salaam. Kampuni ya TECNO Mobile Limited imezindua uwanja wa kisasa katika eneo la Mwananyamala utakaokuwa ukitumiwa na vijana na watoto kukuza vipaji vya mpira wa miguu katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam.

Kampuni ya  hiyo imewekeza nguvu na malengo ya kukuza tasnia ya mpira wa miguu kwa jamii ya Kitanzania ikiwamo kujenga viwanja na kukuza vipaji vya vijana chini ya umri wa miaka 17 kwenye soka ikiwa ni hatua ya awali.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa uwanja huo uliogharimu zaidi ya Shilingi 70 Milioni, Meneja wa kampuni hiyo nchini Tanzania, Dino Han, alisema kuwa hiyo ni hatua ya kwanza ila kampuni ina mipango thabiti ya kuendelea kuchangia katika maendeleo ya mpira wa miguu nchini Tanzania kwa kujenga viwanja vya kisasa vingi zaidi kupitia mauzo ya bidhaa zake ikiwamo simu za mkononi.

Akitoa shukrani kwa wakazi wa Mwananyamala kwa kukubaliana na  jitihada zao za kuboresha kiwanja hicho ambacho kwa sasa kina muonekano wa kisasa alisema.

 “Tunawashukuru viongozi wa Serikali pamoja na wazazi wa Mwananyamala kwa kukubali kiwanja hiki kuboreshwa ili kukidhi soka la awali kwa vijana wao, lengo letu ni kuendeleza mauzo ya bidhaa zetu ili kuboresha viwanja vingine zaidi,”alisema.   

Katika hatua nyingine ya kukuza mpira wa miguu kwa vijana, meneja huyo alisema kupitia mpango wa Watoto wa Power Tanzania Moment watoto 20 wamechaguliwa kujiunga na Academy ya Hornet ya Masaki jijini Dar es Salaam, ambapo watajifunza kwa miezi mitatu, pia wazazi wao watakabidhiwa Shilingi 3 milioni kwa ajili ya kukidhi mahitaji yao na kuwa motisha ili kuendeleza vipaji vyao.

“Pesa hizi zimetokana na mauzo ya simu ya mwezi Desemba, mwaka jana, kila simu iliyouzwa  shilingi  10,000 ilitengwa kwa ajili ya kukuza vipaji vya mpira wa miguu, ambapo zilipatikana 90 Milioni,” alisema meneja huyo.

Kwa Upande wa Meya wa Kinondoni, Songoro Mnyonge aliishukuru Kampuni ya TECNO mobile limited kwa hatua yake ya kukuza soka nchini kwa vijana, huku akizitaka kampuni nyingine na wadau kuwekeza katika soka la vijana.

“TECNO iwe mfano kwa makampuni mengine katika jitihada za kukuza soka letu kuanzia kwa vijana, soka ni ajira na hatunabudi kutengeneza vipaji kuanzia kwa vijana wadogo. Suala la kuboresha miundombinu ya viwanja vyetu ni muhimu sana,”alisema meya huyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *