Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameyataja mashambulizi haya yaliyoongezeka kuwa ukiukwaji usiokubalika wa sheria za kimataifa za kibinadamu.
Wafanyakazi wawili wa UNHCR wanaangalia jengo la makazi lililoharibiwa huko Dnipro, Ukraine.
Pakistan: Sheria za kibinadamu lazima ziheshimiwe
Mwakilishi wa Pakistan amekumbusha kuwa mwezi Februari unaashiria miaka minne tangu kuanza kwa mgogoro wa Ukraine, akisema jumuiya ya kimataifa ina wasiwasi mkubwa kuhusu kuendelea kwa mapigano makali.
Ameeleza kuwa ongezeko la hivi karibuni la mashambulizi limezidisha hali mbaya ya kibinadamu, na kusisitiza kuwa ulinzi wa raia na miundombinu ya kiraia ni msingi wa sheria za kimataifa za kibinadamu, ambazo lazima ziheshimiwe kikamilifu na pande zote.
Marekani: Mashambulizi ni ongezeko lisiloelezeka la vita
Mwakilishi wa Marekani amesema kutokana na uongozi wa Rais Trump, dunia iko karibu zaidi na makubaliano ya amani kuliko wakati wowote tangu vita vilipoanza.
Hata hivyo, amelaani mashambulizi ya Urusi dhidi ya Ukraine, yakiwemo makombora yenye uwezo wa kubeba silaha za nyuklia, akiyataja kuwa ni “ongezeko hatari na lisiloelezeka” la vita.
Amesema kushambulia raia na miundombinu ya nishati ni “kejeli kwa lengo la amani”.
Moshi ukisambaa kutoka kwa jengo la makazi huko Kyiv kufuatia shambulio la usiku.
China: Mgogoro wa Ukraine usitumike kuweka vikwazo
China imesema fursa ya mazungumzo imefunguka na mlango wa amani unaonekana. Mwakilishi wake amehimiza pande zote kujenga juu ya mafanikio ya duru ya hivi karibuni ya mazungumzo.
Amepinga vikali juhudi za kutumia mgogoro wa Ukraine kama kisingizio cha kuweka vikwazo vya upande mmoja visivyo halali na kuvuruga biashara ya kimataifa.
Denmark: Kushambulia raia ni uhalifu wa kivita
Denmark imelaani vikali mashambulizi ya Urusi, ikisisitiza kuwa kuelekeza mashambulizi dhidi ya raia ni uhalifu wa kivita.
Mwakilishi wake amesema kushambulia miji iliyo karibu na maeneo ya NATO na Muungano wa Ulaya ni ishara ya uzembe wa Urusi na chanzo cha wasiwasi mkubwa kwa usalama wa kikanda.
Liberia: Mkataba wa Umoja wa Mataifa uheshimiwe
Liberia imesema vita vya Ukraine vinajaribu misingi ya Umoja wa Mataifa, ambayo ni kanuni zinazowezesha mataifa kuishi kwa amani.
Mwakilishi wake ameonya kuwa kupuuzwa au kutumika kwa kuchagua kwa kanuni hizi kumeufanya ulimwengu kuwa hatari zaidi, na kusisitiza kuwa matumizi ya nguvu si lugha halali ya usalama.
Amehimiza pande zote kuheshimu wajibu wao chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
Latvia: Urusi inajaribu dhamira ya kimataifa
Latvia imetoa wito kwa Baraza la Usalama kulaani “ukatili wa kimfumo” wa Urusi.
Mwakilishi wake amesema mashambulizi dhidi ya raia wa Ukraine wakati wa baridi kali kali ni jaribio la makusudi la kupima uvumilivu wa jumuiya ya kimataifa.
Ameongeza kuwa Ulaya imefanya kazi kwa dhati kurejesha amani barani humo.
Mwanamke mmoja mzee anatafakari juu ya uharibifu wa nyumba yake huko Staryi Saltiv, mashariki mwa Ukraine.
Hali ya raia yazidi kuwa mbaya
Ramesh Rajasingham, Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya dharura na misaada OCHA mjini Geneva, amesema hali ya raia nchini Ukraine imekuwa mbaya zaidi.
Akizungumza kwa niaba ya Mratibu wa Misaada ya Dharura Tom Fletcher, amesema Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) limeripoti mashambulizi 11 dhidi ya vituo vya afya tangu mwanzo wa mwaka.
Ameonya kuwa uharibifu wa vituo vya umeme, mabomba ya joto na vituo vya maji unasababisha mfululizo wa matatizo yanayohatarisha maisha ya watu zaidi.
Amehimiza wajumbe wa Baraza la Usalama kutumia sauti, ushawishi na uhusiano wao kuhakikisha raia wanalindwa, misaada ya kibinadamu inawafikia bila vikwazo, na ufadhili unaendana na kiwango cha mahitaji.
“Raia wanaopitia mashambulizi haya wanahitaji zaidi ya kauli za wasiwasi,” amesema.
Mwaka mpya haujaleta amani
Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya kisiasa na ujenzi wa amani, Rosemary DiCarlo, yeye amema mwanzo wa mwaka mpya haujaleta amani wala mapumziko kwa Ukraine.
Amesema mashambulizi makubwa ya anga dhidi ya raia na miundombinu ya kiraia yamesababisha uharibifu na mateso makubwa.
Kati ya tarehe 8 na 9 Januari, Urusi iliripotiwa kurusha ndege zisizo na rubani 242 na makombora 36 dhidi ya Ukraine, na kusababisha vifo vya watu wasiopungua wanne na majeruhi 25 mjini Kyiv.
Maeneo ya Lviv pia yalilengwa kwa silaha inayojulikana kama Oreshnik, inayodhaniwa kuwa na uwezo wa kubeba silaha za nyuklia.
DiCarlo amesisitiza wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kusitishwa mara moja kwa mapigano bila masharti yoyote, akisema amani yoyote lazima iheshimu kikamilifu uhuru, mamlaka na mipaka ya Ukraine inayotambulika kimataifa.
