Taarifa ya ujumbe huo kutoka Geneva Uswisi na Panama imeeleza kuwa “hatua yoyote inayorejesha uhuru kwa watu waliokamatwa kiholela ni muhimu sana, si tu kwa waliokombolewa bali pia kwa familia zao, ambazo kwa muda mrefu zimevumilia hali ya kutokuwa na uhakika, mateso na maumivu makubwa ya kisaikolojia huku zikiendelea kupigania haki za wapendwa wao.”

Hata hivyo, kati ya makadirio ya wafungwa wa kisiasa wapatao 800, ni takribani watu 50 pekee ndio walioachiliwa hadi sasa, wakiwemo baadhi ambao kesi zao zimeainishwa katika ripoti za awali za Ujumbe huu na ujumbe wa UN umeeleza hiyo ni hatua ndogo. 

“Hatua hii bado iko mbali na kutimiza wajibu wa Venezuela chini ya sheria za kimataifa za haki za binadamu. Ujumbe unaendelea kuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu wanawake waliobaki rumande, kutokana na athari kubwa wanazokumbana nazo kiafya pamoja na majukumu yao ya malezi.”

Ukamataji unaendelea

Ujumbe huu umeeleza kwenye taarifa yake wamebaini kwa kina matumizi ya kukamatwa kiholela kama chombo cha ukandamizaji wa kisiasa na wametoa wito kwa serikali “tunasisitiza wito wa kuachiliwa mara moja na bila masharti kwa wafungwa wote wa kisiasa na watu wote waliopokonywa uhuru wao kinyume cha sheria. Aidha, mahitaji ya kiafya ya waliokwisha achiliwa lazima yashughulikiwe haraka.”

Pia wameeleza kuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu mateso yanayoendelea kwa familia za wafungwa. “Serikali inapaswa kutoa taarifa kwa uwazi na kwa wakati kuhusu hatma, mahali walipo na hali ya kisheria ya wafungwa, pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa fursa ya wafungwa hao kutembelewa na wapendwa wao mara kwa mara. Kuwekwa kizuizini bila mawasiliano ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na lazima kukomeshwe mara moja.”

Wameongeza kuwa “tunazitaka mamlaka za Venezuela kuchukua hatua za haraka na kwa uwazi, ikiwemo kutoa taarifa za umma kuhusu mipango ya kuachiliwa zaidi, vigezo vinavyotumika na ratiba husika. Wakati huo huo, hali za vizuizini lazima zilingane na sheria za kimataifa, ikijumuisha upatikanaji wa huduma za afya, mawakili, familia, na kusitishwa mara moja kwa mateso na vitendo vyote vya kikatili, visivyo vya kibinadamu au vya kudhalilisha.”

Ujumbe unaendelea kufuatilia kwa karibu hali inayoendelea nchini Venezuela na unabaki na wasiwasi kuwa mazingira mapana ya ukandamizaji bado yanaendelea. Wameeleza kuna haja ya dharura ya kukomesha vitendo vyote vya ukandamizaji na kuweka haki za binadamu mbele. “Jumuiya ya kimataifa lazima iweke shinikizo hilo kuwa kipaumbele katika kipindi hiki muhimu.”

Kuhusu ujumbe wa kusaka ukweli nchini Venezuela 

Mwezi Septemba 2019, Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu lilianzisha Ujumbe Huru wa Kimataifa wa Kutafuta Ukweli kuhusu Jamhuri ya Venezuela ili kutathmini madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa tangu 2014. 

Ujumbe wa Kutafuta Ukweli uliwasilisha ripoti yake ya hivi karibuni ya mwaka wakati wa mazungumzo shirikishi katika Baraza mwezi Septemba 2024, ripoti ambayo iliambatanisha matokeo yote waliyofanyia uchunguzo kwa kina. 

Katika azimio lake namba 57/36, Baraza liliongeza muda wa Ujumbe wa Kutafuta Ukweli kwa miaka miwili zaidi, hadi mwezi Oktoba 2026.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *