
Wito huo umetolewa leo Januari 12 na unahusu ulimwengu mzima, kwa msisitizo maalum katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro na majanga ya kibinadamu.
McCain amesisitiza kuwa hatua hizo ni za dharura kwa kuwa mamia ya mamilioni ya watu kwa sasa wanakabiliwa na viwango hatarishi vya njaa. Ameeleza kuwa suluhisho linahitaji uongozi thabiti wa kisiasa, ufadhili wa haraka, pamoja na utekelezaji wa hatua za mapema za kibinadamu ili kuzuia hali ya njaa kuendelea kuathiri maisha na uthabiti wa jamii.
“Takribani wiki mbili tu tangu kuanza kwa mwaka mpya, dunia tayari inakabiliwa na hatari ya mgogoro mkubwa na unaozidi kuimarika wa njaa duniani, azma ya WFP bado ni thabiti. Tutatumia kila fursa kuhamasisha uungwaji mkono na rasilimali zinazohitajika kuwafikia wale wanaotutegemea kwa ajili ya kuendelea kuishi.” amesisitiza Bi. McCain.
Taarifa hiyo iliyotolewa jijini Roma, Italia inasema kuwa mkuu huyo wa WHO, McCain atahutubia timu ya kimataifa ya WFP katika mkutano utakaofanyika katika makao makuu ya shirika hilo mjini Roma, Italia, akieleza vipaumbele vya juu vya kukabiliana na njaa mwaka 2026. Vipaumbele hivyo ni pamoja na kupanua wigo wa ufadhili wa WFP, kutumia kikamilifu uwezo wa mabadiliko unaotokana na teknolojia mpya, na kuhakikisha timu zilizo mstari wa mbele zinapata msaada unaohitajika kufanya kazi zao kwa usalama na ufanisi. McCain atasisitiza pia umuhimu wa mpango mkakati wa miaka minne wa shirika hilo, uliopitishwa hivi karibuni kwa makubaliano na Bodi ya Utendaji ya WFP, ambao unaipa WFP uwezo wa kufikia athari chanya kubwa zaidi kwa ufanisi wa juu.
Mkurugenzi Mtendaji wa WFP, ambaye husafiri mara kwa mara katika maeneo hatarishi ya migogoro na maeneo yenye dharura kubwa duniani, atasisitiza kuwa kuwafikia watu walio hatarini zaidi kwa haraka, pamoja na kuongeza athari na ufanisi katika mazingira yanayozidi kuwa magumu, ni jambo la muhimu zaidi kuliko wakati mwingine wowote.
“WFP imethibitisha mara kwa mara kuwa suluhisho za mapema, za kimkakati na za ubunifu zinaweza kuzuia njaa kali, kuimarisha jamii, kupunguza uhamiaji wa kulazimishwa na kusaidia familia kurejea katika hali ya kawaida,” anasema Mkurugenzi Mtendaji McCain.
Hata hivyo, makadirio ya sasa yanaonesha kuwa ufadhili wa WFP uko chini ya nusu ya bajeti yake inayohitajika ya dola za Marekani bilioni 13, inayolenga kuwafikia watu milioni 110 walio katika hatari kubwa zaidi duniani. Wakati huohuo, mazingira ya kazi yanayozidi kuwa magumu na hatarishi yanafanya kazi za kibinadamu kuwa ngumu na hatari zaidi. Kutokana na hali hiyo, mamilioni ya watu wako katika hatari ya kukosa msaada muhimu wa kuokoa maisha, jambo linalohatarisha maisha yao na uthabiti wa maeneo mbalimbali.
Mkurugenzi Mtendaji McCain, ambaye huzungumzia mara kwa mara uhusiano kati ya njaa na migogoro, amewataka viongozi wa dunia kuweka kipaumbele katika kushughulikia ukosefu wa usalama wa chakula duniani na kuzuia njaa zinazosababishwa na binadamu.
McCain amesema kuwa WFP haiwezi kumaliza njaa peke yake. Migogoro ya leo inahitaji hatua za haraka, za kimkakati na zenye maamuzi. Anawataka viongozi wa dunia kuchukua hatua mapema zaidi wakati wa majanga ya kibinadamu, kuondoa kabisa njaa zinazosababishwa na binadamu, na muhimu zaidi, kukomesha migogoro hii ya uharibifu inayochochea njaa na kukata tamaa.