Dar es Salaam. Mwigizaji wa filamu nchini, Steven Charles ‘Dk Alsmas’ amefunga mjadala wa maswali kuhusiana na hereni anazovaa.
Almas mwenye umri wa miaka 62, amesema ukiachilia mbali usanii, pia anavaa hereni kwa sababu ya kufuata mila na tamaduni za Mwafrika na kutaja baadhi ya makabila ambayo bado yanaendeleza utamaduni huo.
“Uvaaji wa hereni kwa Mwafrika ni asili yake watu wengi hawajui. Watu historia wameidandia hapa mbele mababu zetu waliokamatwa wakauzwa utumwani kwenda Amerika, Ulaya, na maeneo yote ya dunia waliondoka huku wanavaa hereni. Mfano Wagogo wanavaa hereni, Wamaasai, Wasukuma wanavaa hereni mpaka kesho. kwa ushuhuda huo watu watajua huyu mzee anajua anachokifanya,” amesema Almas.
Almas amesema licha ya ubishoo wake kabla ya kuwa mwigizaji amewahi kufanya kazi kama mhudumu wa Hoteli na kondakta wa malori
“Mimi nimefanya kazi kibao kabla ya kuwa muigizaji. Nimeshakuwa tingo wa kwenye maroli baadaye ndio nikasema embu ngoja nikasome Hotel Management. nimeshakuwa Meneja wa Hotel, nimeshakuwa muhudumu wa kawaida wa Hotel nikawa msimamizi wa hotel.
“Mastaa kipindi hicho walikuwa wachezaji wa mpira wa miguu, Watangazaji wa Radio, Mabaharia kwasababu kipindi chetu wakati tunakuwa vijana mpango mzima ulikuwa ni kuondoka nchini kuchukua meli. Watu wengi walikimbilia nchi kama Ulaya na Amerika wengine tukaishia Zambia, na Afrika Kusini,”amesema.
Amesema amekuwa staa katika maisha yake yote huku akikumbuka kipindi hicho watu walimtunga jina la Steve Wonder. Amesema amewahi kuvunja mkataba wa kuigiza tamthilia ya moja baada ya kulipwa pesa ndogo hali iliyopelekea kufungiwa kuanzia 2017 hadi 2021.
“Ndio na hiyo ndio imeniletea ugomvi na maprodyuza mbalimbali, ilikuwa tamthilia ya (anaitaja) niliitema na ikaishia hapo wakajaribu kushuti sesson 2 wakaipeleka chaneli nyingine, lakini wakaipiga chini kwasababu mimi ndio nilikuwa nimeibeba stori alafu jamaa wamezingua wanataka kunipa hela ndogo, tofauti na nilivyotakiwa kulipwa.
“Nilitakiwa kulipwa Sh8 milioni jamaa akawa ananiletea milioni 5 nikazitema watu wengine waliniona kama mwendawazimu nimetema milioni tano na sikuwa na hela. Naweza kusema haikuendelea kwasababu sikuwepo, wakajaribu kumuweka mwigizaji mwingine lakini haikuendelea,” amesema Almasi.
