India. Tasnia ya muziki wa India hasa unaotumika katika filamu za Bollywood, imekuwa na mifumo na miiko yake. Kwa muda mrefu, kumekuwa na mgawanyo mkubwa kati ya waimbaji na waigizaji.
Mwimbaji anaimba studio, kisha mwigizaji au mrembo mwingine anapewa nafasi ya kuwa video vixen kwenye wimbo huo. Wasanii kama Kajol, Kareena Kapoor, Shah Rukh Khan, Amitabh Bachchan na wengineo wanaoonekana kwenye nyimbo mbalimbali, wao hukaririshwa ngoma hizo lakini wanaoimba wanakuwa nyuma.
Kuna baadhi ya nyimbo ambazo Kajol aliimba kupitia sauti za wakongwe kama Alka Yagnik, Lata Mangeshkar, Sadhana Sargam na wengineo ambao baadhi ya mashabiki waliamini staa huyo wa filamu za Bollywood aliimba mwenyewe.
Nyimbo nyingi za zamani zilizoimbwa na wakongwe kama Udit Narayan zimewapa umaarufu mkubwa waigizaji wa India akiwemo Shah Rukh Khan.
Hata hivyo, mwimbaji wa India, Neha ameibuka na kuanza kuvunja miiko hiyo kwa vitendo, kupitia mtindo wake wa uimbaji. Mwanadada huyo analeta mabadiliko makubwa katika namna muziki wa India unavyotazamwa na kupokelewa.
Neha ni nani?
Jina lake ni Neha Kakkar Singh alizaliwa India mwaka 1988, alianza kuimba mwaka 2005 aliposhiriki katika msimu wa pili wa shindano la kuimba la runinga Indian Idol na aliondolewa mapema katika mashindano hayo.
Hata hivyo, hakukata tamaa na miaka mitatu baadaye alizindua albamu yake ya kwanza iitwayo Neha The Rockstar, ikiwa na muziki uliotungwa na Meet Bros Anjjan.
Katika kipindi hicho, pia alirekodi nyimbo kwa ajili ya albamu ya Romeo Juliet, iliyotungwa na kaka yake, Tony Kakkar. Aliimba wimbo ‘Hai Rama’ kutoka kwenye filamu Meerabai Not Out (2008) pamoja na Sukhwinder Singh.
Tangu hapo hadi sasa ameendelea kuimba na mara kadhaa amekuwa akionekana kwenye filamu mbalimbali za India.
Mbali na kuimba na kuigiza lakini amekuwa jaji kwenye mashindano makubwa ya kutafuta vipaji nchini humo ya Indian Idol.
Anaimba na kuonekana kwenye video
Katika muziki wa India, ilikuwa kawaida kuona mwimbaji haonekana kwenye video. Kazi yake ilikuwa ni kuimba tu, huku waigizaji maarufu au warembo wakipewa nafasi ya kuonekana lakini mwanadada huyo ni huonekana mwenyewe kwenye kazi zake, ndiyo maana tunasema amevunja miiko.
Neha huimba na huonekana moja kwa moja kwenye video za nyimbo zake. Yeye ndiye sauti, sura na mhusika mkuu wa wimbo. Hii ni tofauti na ilivyozoeleka India, lakini inafanana zaidi na muziki wa kimataifa na msanii ndiye anayeongoza kila kitu kwenye kazi yake.
Nyimbo kama Dilbar, O Saki Saki, Aankh Marey na Coca Cola, Tu Pyaasa Hai Neha anaonyesha mwimbaji anaweza kuwa pia mwigizaji wa wimbo wake. Hii imewapa msukumo baadhi ya wasanii wengine wa kizazi kipya India.
Wasanii wakubwa kama Shreya Ghoshal, Lata Mangeshkar na Alka Yagnik waliimba nyimbo nyingi bila kuonekana kwenye video. Neha hakupinga mfumo huo kwa maneno, bali kwa vitendo. Alianza kukubali nyimbo ambazo angeweza kuonekana mwenyewe hii ilionekana kama jambo geni mwanzoni, lakini mashabiki wake kwa sasa wamezoea.
Familia ya muziki
Neha anatoka katika familia yenye mizizi ya muziki. Dada yake, Sonu Kakkar, ni mwimbaji aliyemfungulia njia katika tasnia hiyo. Kaka yake, Tony Kakkar, ni mtunzi na mwimbaji wa nyimbo nyingi maarufu.
Familia hii imekuwa ikipeana msaada mkubwa, jambo ambalo limechangia mafanikio ya Neha. Tony ameandika na kutunga nyimbo nyingi ambazo Neha amezifanya kuwa maarufu.
Hata hivyo, dada yake Sonu alifuata utaratibu ule wa kuwa playback singer lakini baada ya Neha kuanza kubadilika na kaka yake Tony amefuata nyayo hizo.
Mahusiano
Neha aliwahi kuwa kwenye uhusiano uliotikisa kwenye mitandao ya kijamii na mwimbaji Himansh Kohli. Waliyekutana wakati wa kurekodi wimbo Yaad Piya Ki Aane Lagi. Hata hivyo, uhusiano huo uliisha kwa maumivu. Ambapo Neha aliwahi kuweka wazi kupitia nyimbo na mahojiano akieleza kuwa alipitia kipindi kigumu cha msongo wa mawazo na huzuni kubwa ya mapenzi.
Baada ya hapo, mwaka 2020, alitangaza ndoa yake na mwimbaji Rohanpreet Singh, jambo lililowashangaza wengi kutokana na kasi ya uamuzi huo. Wawili hao walifunga ndoa tarehe 24 Oktoba 2020.Tangu wakati huo, Neha na Rohanpreet wamekuwa na uhusiano mzuri huku wakishirikiana kurekodi nyimbo kwa pamoja ikiwemo Nehu Da Vyah, Baarish Mein Tum, Gaadi Kaali, Buhe Vich na nyinginezo.