Ndege ya Diddy mikononi mwa tajiri mpya MarekaniNdege ya Diddy mikononi mwa tajiri mpya Marekani

Marekani. Msanii na mfanyabiashara kutoka Marekani, Sean “Diddy” Combs, ameripotiwa kuuza ndege yake binafsi (private jet) aina ya Gulfstream G550, ikiwa ni takribani mwaka mmoja tangu akumbane na kesi zilizopelekea kifungo cha miaka minne jela.

Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na vyombo vya habari Marekani, ndege hiyo yenye rangi nyeusi (matte black) haipo tena chini ya umiliki wa Diddy na tayari imesajiliwa kwa jina jipya.

Hatua ya kuuza ndege hiyo inatajwa ni kutokana na gharama kubwa ambazo anadaiwa na mawakili pamoja na faini aliyotakiwa kutoa. Hata hivyo watu wa karibu na Diddy wanadai uamuzi huo umelenga kuepuka gharama za ndege hiyo ambayo hutumia mamilioni ya dola kwa matengenezo, mafuta na kuwalipa wafanyakazi.

Ingawa thamani halisi ya mauzo haijawekwa wazi, ndege aina ya Gulfstream G550 mara nyingi huuzwa kwa mkwanja mrefu, na ni kulingana na mwaka uliyotengenezwa na ubora wake. 

Jarida la People linaeleza mauzo ya ndege hiyo yameibua mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii baadhi ya mashabiki wakitafsiri hatua hiyo kama dalili ya kuanza kufilisika kwa mkali huyo wa hip hop.

Diddy pamoja na familia yake ni kama wameuanza mwaka 2026 vibaya kwani mapema wiki hii watoto wake waliripotiwa kuishi maisha magumu kutokana na sasa hawawezi kutumia fedha za baba yao kama ambavyo walikuwa wakitumia hapo awali na kuwa wanaishi katika bajeti maalumu.

Fedha na mali zote za Diddy zipo chini ya uangalizi mkali, wa kampuni ya usimamizi wa biashara ya Tri Star Sports & Entertainmen ambao hutoa fedha kwa familia kulingana na bajeti maalumu.

Utakumbuka Oktoba 3, 2025 Diddy alihukumiwa miezi 50 jela (Zaidi ya miaka 4) pamoja na faini ya dola 500,000 kwa makadirio nyota huyo wa ‘I’ll Be Missing You’ anatarajiwa kumaliza kifungo Mei 8,2028.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *