Baada ya kuinoa timu ya taifa ya Rwanda ‘Amavubi’ kwa miezi 10, Kocha Adel Amrouche ameondolewa katika kibarua hicho na Shirikisho la Mpira wa Miguu Rwanda (FERWAFA) jana, Jumanne, Januari 13, 2025.
Uamuzi wa kuachana na Amrouche aliyewahi kuinoa timu ya taifa ya Tanzania kabla ya kujiunga na Amavubi, Machi 2, 2025 umetajwa kusababishwa na kitendo cha kocha huyo kukiuka masharti ya mkataba na Shirikisho hilo ambayo hata hivyo hayajawekwa wazi.
“Shirikisho la Mpira wa Miguu Rwanda (FERWAFA) linatangaza kusitishwa kwa mkataba wa Adel Amrouche kama kocha mkuu wa timu ya taifa ya soka ya wanaume ya Rwanda.
“Uamuzi huu umefuatia tathmini ya kina ya ukiukwaji mkubwa wa masharti ya mkataba kama ilivyobainishwa katika kifungu cha 17.2 cha mkataba wa ajira.
“Amrouche alipewa muda wa kutosha kushughulikia masuala haya kabla ya uamuzi huu kufanyika. Tunamshukuru Amrouche kwa mchango wake kwa shirikisho na tunamtakia kila la heri katika shughuli zake za baadaye,” imefafanua taarifa ya FERWAFA.
Amrouche ametimuliwa huku akiwa amebakiza miezi 14 katika mkataba wake wa kuinoa Rwanda ambayo alishindwa kuiongoza kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026.
Kabla ya kuinoa Rwanda, Amrouche alikuwa akiifundisha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ lakini hata hivyo mkataba wake ulisitishwa Machi mwaka jana.
Adel Amrouche ni nani?
Adel Amrouche alizaliwa Algiers, Algeria, Machi 7, 1968 na alianza maisha yake ya soka katika timu ya vijana ya CR Belouizdad mwaka 1983.
Baadaye alihamia JS Kabylie kabla ya kuanza rasmi soka la kulipwa akiwa na OMR El Annasser mwaka 1988.
Baadaye aliichezea USM Algiers. Pia aliwahi kucheza katika klabu ya Favoritner AC ya Austria, pamoja na Raal La Louvière ya Ubelgiji.
