Raia nchini Uganda wanajiandaa kupiga kura kesho Alhamisi katika uchaguzi ambao unatarajiwa kuwa na ushindni mkubwa baina ya upinzani na rais wa muda mrefu Yoweri Museveni.
Rais Museveni aliyepo madarakani tangu mwaka 1986 anawania awamu ya 7, na kukaribia miongo mitano ya kutawala.
Hata hivyo anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Bobi Wine anayewakilisha kundi la vijana wanaoshinikiza mageuzi ya kisiasa.
Wagombea wengine sita wanawania nafasi ya urais kwenye taifa hilo la Afrika Mashariki lenye karibu watu milioni 45, na kulingana na Mamlaka za uchaguzi, watu milioni 21.6 wamejiandikisha kupiga kura.
Wakati hayo yakiendelea Serikali ya Uganda imeyafungia mashirika yasiyo ya kiserikali 10, huku ikieleza sababu za kuchukua hatua hiyo.
Uamuzi wa kusitisha kwa muda usiojulikana shughuli za baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) nchini humo, umefanyika ikiwa ni siku moja kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu kesho.
