Mipango inaendelea kupangwa kuhakikisha wajumbe wa kamati ya wateknokrati iliyoteuliwa kuendesha masuala ya Ghaza kusafiri hadi Misri kwa mkutano wake wa kwanza, uliotarajiwa kufanyika leo Alkhamisi au kesho Ijumaa. Hayo ni kwa mujibu wa chanzo kimoja cha habari cha Palestina.

Kamati hiyo ni sehemu ya mpango wa kiutawala wa baada ya vita uliopendekezwa na Rais wa Marekani Donald Trump kufuatia vita vya kinyama na mauaji ya kimbari yaliyofanywa na utawala wa kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ghaza, ambavyo vimewaua shahidi zaidi ya Wapalestina 71,000 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 171,000 tangu Oktoba 2023 hadi sasa.

Chanzo hicho kimeeleza kwamba, wajumbe hao wamearifiwa rasmi kuhusu uteuzi wao na wataanza kuhudumu katika nyadhifa husika mara tu jopo hilo litakapokutana mjini Cairo.

Gazeti la New York Times liliripoti wiki hii kwamba Washington inakaribia kutangaza uundwaji wa kamati hiyo, huku naibu waziri wa zamani wa mipango wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina Ali Shaath akitarajiwa kuwa mwenyekiti wake.

Jopo hilo linawaleta pamoja wasomi, wataalamu na watu mashuhuri wa asasi za kiraia waliochaguliwa kutokana na utaalamu wao ili kusimamia sekta muhimu zaidi za Ghaza wakati huu ambapo eneo hilo la Palestina lililowekewa mzingiro linakabiliwa na hali mbaya ya kibinadamu ambayo halijawahi kuishuhudia.

Kutokana na vita vya miaka miwili, utawala wa kizayuni wa Israel umeharibu karibu asilimia 90 ya miundomsingi ya Ghaza, huku Umoja wa Mataifa ukikadiria gharama za ujenzi mpya wa eneo hilo kufikia takribani dola bilioni 70.

Kwa mujibu wa mpango huo wa vipengele 20 uliopendekezwa na Trump, chombo hicho cha uendeshaji cha wateknokrati kitafanya kazi chini ya usimamizi wa kile kinachoitwa “Baraza la Amani” ambalo litaongozwa na rais huyo wa Marekani na kuhusisha pia watu mashuhuri kadhaa kimataifa ambao bado hawajatajwa.

Hayo yanajiri sambamba na mjumbe maalumu wa Trump, Steve Witkof kutangaza siku ya Jumatano kuanza kwa awamu ya pili ya mpango wa kusitisha mapigano Ghaza, akisema lengo la awamu hiyo litahusu upokonyaji silaha, kuwepo utawala wa kiteknokrati, na kufanyika ujenzi upya wa eneo hilo…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *