
Rais wa Marekani Donald Trump ameonekana kwenye mkanda wa video akimtukana tusi la nguoni mfanyakazi mmoja wa kampuni ya magari ya Ford Motor aliyemkosoa kiuchokozi wakati alipotembelea kiwanda kimoja cha kampuni hiyo kilichoko karibu na mji wa Detroit.
Mfanyakazi huyo aliyetambuliwa kwa jina la TJ Sabula mwenye umri wa miaka 40 alimwita Trump ‘mlindaji wa mharibifu wa watoto’ akimaanisha hatua ya rais huyo wa Marekani ya kukwamisha kuwekwa hadharani nyaraka na taarifa zote zinazomhusu Jeffrey Epstein, aliyepatikana na hatia ya kufadhili kifedha biashara haramu ya ngono dhidi ya watoto wadogo na aliyefia jela kwa kujiua katika gereza la New York mnamo 2019 wakati anasubiri kupandishwa kizimbani kwa kesi iliyokuwa ikimkabili ya biashara hiyo haramu ya ngono.
Kifo cha Epstein kilizua shaka na utata mwingi kwamba aliuawa ili kuzuia ushuhuda kuhusu uhalifu wa vitendo hivyo haramu vya ngono dhidi ya watoto unaodaiwa kuwahusisha watu mashuhuri akiwemo Trump mwenyewe.
Kwa mujibu wa mkanda wa video uliosambaa mitandaoni, baada ya Trump kuchokozwa kwa kuitwa mlindaji wa mharibifu wa watoto, alimgeukia Sabula na kumtolea matusi kadhaa pamoja na harakati ya kuinua kidole chake cha kati. Inasemekana, rais huyo wa Marekani alitamka pia tusi linalotafsiriwa na harakati hiyo aliyoonyesha.
Licha ya kusimamishwa kazi, mfanyakazi huyo wa kampuni ya Ford Motor amesema: “kuhusiana na nilivyomkosoa, hakuna lolote la kujutia,” na akaongeza kwamba, anaamini “alilengwa ili kulipiziwa kisasi kisiasa” kwa “kumuaibisha Trump mbele ya marafiki zake.”
Hayo yanajiri huku ripoti zikieleza kwamba, Sabula amepata uungaji mkono mkubwa kwa marafiki zake, ambao wameamua kuanzisha kampeni maalumu ya kumchangishia fedha, na hadi wakati huu ameshapata zaidi ya dola laki nane za kimarekani…/