Muungano wa mashirika yasiyo ya kiserikali ya Uingereza (NGOs) umeitaka serikali ya nchi hiyo kusitisha uuzaji wa silaha kwa utawala wa Israel, na kuonya kuwa silaha zinazotengenezwa Uingereza ziko hatarini kutumika katika mauaji ya kimbari na kuzidi kumomonyoa sheria za kimataifa.
Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa jana Ijumaa, makundi matano ambayo ni Campaign Against Arms Trade, Global Justice Now, the Global Legal Action Network, the International Centre of Justice for Palestinians, na War on Want, yamesema yameshtushwa na ishara kwamba serikali inaweza kuondoa vizuizi vya leseni ya kuuza silaha katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na Israel.
Taarifa ya makundi hayo imefuatia maoni ya Waziri wa Biashara wa Uingereza, Peter Kyle, ambaye amesema, uuzaji wa silaha kwa Israel unaweza kuanza tena ikiwa kutakuwapo maendeleo kuhusu kile alichoelezea kama “amani endelevu.”
Muungano wa mashirika yasiyo ya kiserikali ya Uingereza (NGOs) umepinga vikali msimamo huo ukisema “umeenda kinyume kabisa na ukweli wa mambo,” ukiashiria ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano unaoendelea kufanywa na Israel.
“Msimamo wa Serikali ulikuwa tayari haukubaliki,” imesema taarifa hiyo, ikisisitiza kwamba Uingereza imesitisha karibu leseni 30 kati ya takriban 350 za kuuza silaha kwa Israel, ambayo ni asilimia 8.6 tu ya jumla ya mauuzo yote ya silaha kwa utawala huo.
Mnamo Septemba 2024, serikali ya Uingereza ilitangaza kusimamishwa uuzaji silaha mdogo kwa Israel baada ya ukaguzi kubaini kwamba silaha zinazotengenezwa Uingereza zinaweza kutumika kutekeleza au kuwezesha ukiukaji mkubwa wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu huko Palestina. NGOs zimesisitiza kuwa hali ya mambo huko Gaza imekuwa mbaya zaidi tangu wakati huo.
Muungano wa mashirika yasiyo ya kiserikali ya Uingereza (NGOs) uumesema hatua za Israel zinaonyesha “kutojali kabisa amani” na kwamba ni kielelezo cha mwendelezo wa mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Palestina, na kwamba hatua yoyote ya kuanza tena mauzo ya silaha kwa utawala huo haiwezi kutetewa kimaadili.
Wizara ya Afya ya Gaza inaripoti kwamba Wapalestina wasiopungua 460 wameuawa na karibu 1,270 wamejeruhiwa katika mashambulizi ya Israel tangu kuanza usitishaji mapigano.

Tangu Israel ilipoanzisha mashambulizi yake ya mauaji ya kimbari huko Gaza Oktoba 7, 2023, zaidi ya Wapalestina 71,000 wameuawa na wengine zaidi ya 172,000 wamejeruhiwa, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.