Wasichana mara mingi wameachwa nyuma katika masomo ya TEHAMA, lakini kwa juhudi zao za kusongesha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) vijana wa kike wameweza kushiriki mpango huu wa kujifunza stadi za teknolojia ili waweze kuedeleza biashara ya mtandaoni pamoja na matumizi mengine. Sheilah Jepngetich wa idhaa hii amefuatilia matokeo yake na kutuandalia mada hii kwa kina.
Marua Hub inatarajiwa kuwa mazingira salama na jumuishi ya kukuza ujuzi unaohitajika sokoni na kuwafungulia vijana fursa mpya za maendeleo.
Pamoja na mafunzo ya stadi za kidijitali, wasichana na kina mama vijana wanapata msaada wa vifaa vya kiutu kama hatua ya kwanza ya kuwarejeshea utu wao. Patricia Njeri, Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Birth and Beyond, anaeleza
” Hadi sasa tumewawezesha zaidi ya wasichana 2,000 kwa taulo za kike na nepi. Tumetoa pia vifaa vya kurejesha utu wao kama vile pedi, na pia pakiti za chakula. Tumefanya matukio mengi ya ushauri na uhamasishaji kwa akina mama vijana.”
Wasichana na Wanawake katika ICT katika kituo cha mradi Marua Hub unaolenga kuwawezesha vijana wasichana na kuwapatia eneo salama linalowapatia msaada wa kiutu na kuwajengea uwezo katika eneo la Ongata Rongai, Kaunti ya Kajiado nchini Kenya.
Patricia akaenda mbali kueleza lengo kuu la mradi wa Marua Hub,
“Tunachotarajia kuanzia leo ni kuwa wasichana na kinamama watakuja katikasehemu hii kupata mafunzo, kujengewa uwezo na kupata matumaini mapya kwa ajili ya watoto wao na maisha ya baadaye. Kwa nini Kajiado? Kwa neema ya Mungu nilijikuta nikiishi Kajiado. Lakini pia mradi huu umetokana na ukweli kwamba mimi mwenyewe nilikuwa mama kijana nikiwa na miaka kumi na tisa. Nilijua hili ni eneo ambalo mara nyingi halisaidii wasichana, kwa sababu akina mama vijana hukumbana na aibu na unyanyapaa kutoka kwa jamii. Ndiyo maana niliamua kuwasimama bega kwa bega na kuwasaidia.”
Anne ni mmoja wa wanufaika wa mradi wa Marua Hub, anaeleza jinsi mafunzo ya kidijitali yamemsaidia kukuza ujuzi wake wa teknolojia. Akisema mouse anamaanisha kipanya cha kompyuta,na digital device ni kifaa cha kidijitali.
“Tangu nije kwenye Klabu ya Kompyuta ya Marua Hub, nimejifunza mambo mengi. Nimejifunza kutumia kipanya cha kompyuta. Wakati nilipoanza kuja, sikuwa najua kutumia kifaa cha kidijitali kabisa; sikuwa najua kuunganisha nyaya za umeme, lakini sasa naweza kuziunganisha na kuwasha vifaa. Tumetengeneza barua pepe, tumeandika nyaraka, na nimejifunza angalau kuandika riwaya ndogo. Tunashukuru Marua Hub kwa kutusaidia na vifaa. Kwenye sehemu nyingine unalipa, lakini hapa tumepewa bure, na sasa tumeweza kutumia vifaa vya kidijitali. Tunashukuru sana Marua Hub na Patricia.”
Kituo hicho inawapatia wasichana na akina mama vijana kuingia kikamilifu katika ulimwengu wa teknolojia. Grace Wambua, mkazi wa Rongai na mfanyakazi wa kujitolea wa Birth and Beyond, ambaye ndiye kiongozi wa masuala ya kidijitali anasema
“Dhamira yetu ni kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma katika enzi hii ya kidijitali. Hapa Marua Hub tutakuwa tukitoa kozi mbalimbali. Tunayo mafunzo ya msingi ya matumizi ya kompyuta na pia programu za ofisi. Tutafundisha uundaji wa tovuti, usanifu wa tovuti, pamoja na masomo ya AI.”
Bi. Wambua akaenda mbali kueleza matumaini yao kwa vijana Kajiado.
“Tunataka kuunda nafasi salama ambapo kila mtu ataweza kuketi mbele ya kompyuta kwa kujiamini na kuielewa vizuri. Pia tunataka watu wapate ujuzi wa msingi wa teknolojia wanaohitaji kwa kutumia vifaa vya kisasa tulivyo navyo. Naamini karibu kila mtu sasa anamiliki simu janja. Kwa hiyo hata mbinu rahisi za kurekebisha matatizo yanapotokea kwenye simu yako ukiwa nyumbani wakati haifanyi kazi na hujui la kufanya hizo pia ni stadi tutakazowapa watu wanaokuja hapa. Tunataka wawe na uwezo wa kujua nini cha kufanya wakati wowote kabla hata ya kumtafuta mtaalamu.”
Halikadhallika mradi huu unatarajiwa kuchochea maendeleo ya jamii kwa kuwapa vijana stadi muhimu za kustawi katika uchumi wa sasa. Ann Mercy Wairimu , mwakilishi kutoka Branch International, anasema
“Leo tumepata nafasi nzuri sana ya kujifunza kuhusu wasichana wanaolelewa hapa jinsi wanavyoishi, hatua wanazopitia, na programu wanazoshirikishwa hadi pale wanapoweza kurejea katika jamii, kujitegemea pamoja na watoto wao, na kuwa wanachama wanaochangia maendeleo ya kiuchumi katika jamii. Leo pia ni hatua muhimu sana kwao. Hili ni jambo walilolitamani kwa muda mrefu, na ndio maana sisi kama Branch International tumeshirikiana nao na kuwachangia kompyuta. Tunatumaini kuwa, kwa kuwa tayari tumekutana na baadhi ya wakufunzi wao, mradi huu utakuwa na mafanikio makubwa katika siku zijazo.”