Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Dharura, (OCHA) nchini humo, Paola Emerson, amewaambia waandishi wa habari huko Geneva, Uswisi kuwa majimbo ya Gaza, Sofala na Maputo ndiyo yaliyoathirika vibaya zaidi.

Akizungumzakutoka mji mkuu wa jimbo la Gaza, Xai Xai, Bi. Emerson amesema zaidi ya watu nusu milioni wameathiriwa vibaya na mafuriko hayo, yaliyosababishwa na mvua kubwa katika wiki za mwanzo za mwaka mpya.

Mnamo Januari 19, 2026, wakazi wanatembea kupitia barabara iliyojaa maji huko Xai Xai, mkoa wa Gaza, Msumbiji, baada ya mvua kubwa inayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.

© UNICEF/Guy Taylor

Watu wanatembea barabarani baada ya mvua kubwa kutua huko Xai Xai, jiji lililo kusini mwa Msumbiji.

Mabwawa yaachilia maji ili yasipasuke kingo

“Idadi inaendelea kuongezeka huku mafuriko makubwa yakiendelea na mabwawa yakiendelea kuachilia maji ili kuepuka kupasuka,” na kwamba, “asilimia 90 ya wananchi wa Msumbiji wanaishi katika nyumba zilizojengwa kwa matofali ya udongo, ambazo kimsingi huweza kumomonyoka baada ya siku chache za mvua”.

Vituo vya afya, barabara na miundombinu muhimu pia vimeathiriwa vibaya kwa kiasi kikubwa. Bi. Emerson amesema na kwamba takribani kilomita 5,000 za barabara zimeharibiwa katika majimbo tisa, ikiwemo barabara kuu inayounganisha mji mkuu wa Msumbiji, Maputo na maeneo mengine ya nchi, ambayo kwa sasa haipitiki, hali inayosababisha usumbufu mkubwa katika minyororo ya usambazaji.

Akitoa mfano wa kiwango cha maji kinachoachiliwa na mabwawa ili yasipasuke, Afisa huyo wa OCHA amesema “katika bwawa moja tu, hadi mita za ujazo 10,000 za maji zilikuwa zinaachiliwa. Hii ni takribani mara 25 ya kiasi cha maji ambacho kingeweza kutoshea katika chumba cha mkutano wa waandishi wa habari mlipo leo, kila sekunde,” Bi. Emerson amewaambia waandishi wa habari waliokuwa wamekaa katika chumba chenye uwezo wa zaidi ya watu 100.

“Huwezi kufikiria nguvu ya maji haya na madhara yake kwa watu na miundombinu.”

Hali ya dharura  yatangazwa Msumbiji

Serikali ya Msumbiji imetangaza hali ya dharura ya kitaifa na imeanzisha kituo cha operesheni za dharura katika jimbo la Gaza.

Mji wa Xai-Xai, ulio karibu na Mto Limpopo, umefurika, hali iliyosababisha uhamishaji wa wakazi.

Bi. Emerson amesema mamlaka zimetoa tahadhari kwa maeneo ya katikati ya jiji la Xai-Xai, “ikiwemo onyo la hatari ya mamba katika maeneo yaliyofurika”.

“Viwango vya maji ya mto vinaongezeka na kufikia maeneo ya mijini au yenye watu wengi,” amesema, na kwamba, “mamba walioko katika Mto Limpopo wanaweza kufika katika maeneo ya mijini au yenye makazi ambayo sasa yametwama kwenye maji.”

Mwanachama wa UNICEF anaweka masanduku ya msaada wa dharura katika ghala moja katika mkoa wa Gaza, Msumbiji, ili kukabiliana na mafuriko yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.

© UNICEF/Guy Taylor

Msaada wa dharura uanatayarishwa na mfanyakazi wa UNICEF katika kukabiliana na mafuriko makubwa katika mkoa wa Gaza, Msumbiji.

Maji ya mafuriko na madhara kwa afya ya watoto

Akizungumza pia kutoka Xai-Xai, Mkuu wa Mawasiliano wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) nchini Msumbiji, Guy Taylor, ameonya kuwa mafuriko yanageuza “maji yasiyo salama, milipuko ya magonjwa na utapiamlo kuwa tishio hatari kwa maisha ya watoto”.

Mchanganyiko wa magonjwa ya utapiamlo na  yale yanayoenezwa kupitia maji “mara nyingi unaweza kuwa hatari na kusababisha vifo,” amesema, akisisitiza kuwa hata kabla ya mafuriko, watoto wanne kati ya kila watoto 10 nchini Msumbiji walikuwa wakikumbwa na utapiamlo wa kupindukia.

“Usumbufu huu mpya wa upatikanaji wa chakula, huduma za afya na mbinu za malezi unatishia kuwasukuma watoto walio hatarini zaidi katika mzunguko hatari,” amesisitiza.

Watoto na vijana ndio wanadhurika zaidi

Bwana Taylor ameongeza kuwa Msumbiji sasa inaingia katika msimu wake wa kila mwaka wa vimbunga, hali inayoongeza hatari ya mgogoro maradufu.

“Tunaweza kuzuia magonjwa, vifo na hasara zisizorekebishika kwa watoto, lakini tunahitaji kuchukua hatua haraka,” amesema.

Msemaji huyo wa UNICEF ameitaja Msumbiji kuwa “nchi ya watoto na vijana”, yenye wastani wa umri wa miaka 17.

“Wakati mafuriko na vimbunga vinapotokea, kama ilivyokuwa mara kwa mara na kwa kuongezeka katika miaka ya hivi karibuni, ni watoto na vijana wadogo zaidi wanaoathirika zaidi,” amehitimisha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *