Marekani. Brooklyn Peltz Beckham, mtoto wa kwanza wa nyota wa zamani wa soka David Beckham na mbunifu wa mitindo Victoria Beckham, amevunja ukimya huku akitoa kauli nzito kuhusu mgawanyiko uliopo kwa muda mrefu katika familia yake.

Kufuatia na chapisho aliloweka kwenye mitandao yake ya kijamii Brooklyn amesema alikaa kimya kwa miaka mingi kwa lengo la kulinda faragha ya familia yake. Lakini ameamua kuvunja ukimya huo baada ya familia yake kuendelea kuipotosha jamii katika vyombo vya habari.

“Nimekuwa kimya kwa miaka mingi na nimejitahidi kwa kila njia kuweka masuala haya kuwa ya faragha. Kwa bahati mbaya, wazazi wangu na timu yao wameendelea kwenda kwenye vyombo vya habari, jambo lililoniacha sina budi ila kujisimamia mwenyewe.

“Hivi karibuni nimeona kwa macho yangu mwenyewe ni kwa kiwango gani wako tayari kuweka uongo mwingi kwenye vyombo vya habari, na ninaamini ipo siku ukweli utakuja kugundulika wote,”ameandika Brooklyn

Aidha aliendelea kwa kueleza kuwa hajaamua kuzungumza hivyo kwa nia ya kutaka suluhisho bali ameona ni bora kuvunja uhusiano mazima, hata hivyo amekanusha vikali madai ya kuwa mke wake mwigizaji Nicola Peltz Beckham ndio chanzo cha yeye kugombana na familia yake.

“Mke wangu hanithibiti wala yeye sio chanzo cha yote haya. Kwa mara ya kwanza maishani mwangu, tangu nijitenge na familia yangu, wasiwasi huo umeondoka. Ninaamka kila asubuhi nikiwa na shukrani kwa maisha niliyoyachagua, na nimepata amani na nafuu,” aliandika.

Brooklyn pia alielezea matukio kadhaa ambayo yalifanyika kumdhalilisha mke wake likiwemo la kunyimwa muda wa faragha na David Beckham katika tukio la safari ya London kwa ajili ya kusherehekea siku ya kuzaliwa ya baba yake. Vile vile wanandugu kumkataa mkewe siku ya harusi yao. “Sijawahi kuhisi fedheha na aibu kama ile katika maisha yangu yote,” aliandika.

Katika madai mengine mazito, Brooklyn alisema wazazi wake walimshinikiza kusaini mkataba wa kubadilisha jina la Beckham kabla ya harusi. Alidai kuwa walisisitiza asaini mkataba huo kabla ya sherehe ili masharti ya mkataba yaanze kutekelezwa mara moja.

Aidha mpaka kufikia sasa David Beckham na mkewe Victoria Beckham pamoja na wawakilishi wa familia ya Beckham hawajatoa majibu yoyote kuhusu madai yaliyotolewa na mtoto wao Brooklyn Peltz Beckham.

Utakumbuka familia hiyo ilianza kuingia katika migogoro na mtoto wao mwaka 2022 baada ya kufunga ndoa na Nicola Peltz.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *