
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Radio Okapi ya Umoja wa Mataifa mpango huo unajumuisha hatua za usalama, kisheria na kibinadamu zinazoratibu, kwa lengo la kulinda raia, kulinda mali, na kuimarisha utulivu katika sehemu hiyo muhimu ya nchi.
Tukio la muda mfupi serikali yaonya
Mpango huu unafuatia kuondoka kwa kikosi chenye silaha cha wapiganaji wa AFC/M23, kilichosaidiwa na jeshi la Rwanda kutoka Uvira.
Kwa mujibu wa serikali ya DRC kuondoka huko kwa kwapiganaji hao kumeambatana na uporaji wa mara kwa mara na wizi mkubwa.
Serikali ya Congo imesisitiza kuwa kuondoka kwao hakumaanishi mwisho wa ukatili au kubadilika kweli kwa hali ya usalama kwa ujumla.
Msemaji wa serikali amesema kuondoka kwa M23 ni “tukio la muda mfupi” na akasisitiza kuwa matokeo pekee yanayokubalika ni “kuondoka kikamilifu, kwa ufanisi na bila masharti kwa AFC/M23 na jeshi la Rwanda kutoka katika eneo zima la DRC.”
Vikosi vya usalama vinarudi
Kama sehemu ya kurejesha mamlaka ya Serikali, Vikosi vya Ulinzi vya DRC (FARDC), Polisi ya Taifa ya Congo, na huduma nyingine za usalama vinaendelea kurudi Uvira.
Kazi yao kuu ni kulinda raia, kulinda mali, na kudhibiti athari za “machafuko yaliyopangwa” yaliyoachwa na AFC/M23.
Raia hawahamishwi
Katika taarifa yake ya Jana Jumatatu, 19 Januari, serikali ya DRC pia ilikanusha madai ya uhamisho wa lazima wa raia, hasa wanajamii wa Banyamulenge. Mamlaka ziliashiria kuwa baadhi ya watu walilazimishwa kuondoka Uvira na kundi lenye silaha ili kutumika kama kielelezo cha uwepo wa kikundi hicho kwenye ardhi ya Congo.
Judith Suminwa, mraratibu wa serikali kuhusu masuala ya kibinadamu, ametangaza kuanzishwa tena kwa msaada wa dharura baada ya kuondoka kwa Kundi la M23, kwa lengo la kutoa misaada kwa wananchi walioathirika na kuhakikisha huduma muhimu zinaanza tena.