Naibu mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa ametishia kuichukulia hatua zaidi Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC iwapo itaendeleza uchunguzi wake kuhusu uhalifu na jinai za nchi hiyo.
Jeffrey Bartos, naibu mwakilishi wa Washington katika Umoja wa Mataifa, alitoa tishio hilo katika mkutano wa hivi karibuni wa Baraza la Usalama. Bartos aliendelea na hotuba yake na kusisitiza kuwa Marekani haitairuhusu Mahakama ya Kimataifa ya jinai ICC kuendesha shughuli zake kuhusu nchi hiyo au washirika wake na kuonya kwamba iwapo uchunguzi wa sasa hautasitishwa, Washington itachukua hatua zaidi. Ameitaka mahakama hiyo na nchi wanachama wake kubadilisha mara moja mtazamo wao na kushughulikia kile amekitaja kuwa wasiwasi wa Marekani. Lugha hii kali na isiyo na mfano wake, ambayo ni lugha ya mashinikizo ya kisiasa na sio ya kisheria, inaonyesha wazi kwamba Washington inatekeleza hadharani siasa za mabavu na undumakuwili linapokuja suala la kushughulia taratibu za sheria za kimataifa.
Malalamiko ya Marekani yanaibuliwa katika hali ambayo Mahakama ya Kimataifa ya jinai katika miaka ya karibuni imefungua kesi muhimu ambazo zinahusiana moja kwa moja na vitendo vya uhalifu na jinai vya majeshi ya Marekani nchini Afghanistan, pamoja na ukatili wa Israel katika vita vya Gaza. Uchunguzi kuhusu kamatakamata, operesheni za kijeshi na ukatili wa majeshi ya Marekani nchini Afghanistan kwa upande mmoja na utolewaji wa hati za kukamatwa Benjamin Netanyahu na Yoav Galant wa Israel mwezi Novemba 2024, kwa upande mwingine, umetoa mashinikizo ya ziada dhidi ya Washington. Marekani ambayo siku zote inatoa uungaji mkono mkuwa wa kisiasa, kifedha na kijeshi kwa Israel, sasa inakabiliwa na taasisi ambayo imeamua kufuatilia kesi zinazohusiana na vita vya Gaza bila kujali matokeo ya kisiasa.
Hali hii kwa mara nyingine tena imeanika wazi upendeleo na undumakuwili wa muda mrefu katika siasa za nje za Marekani. Katika uga wa kimataifa, Washington inajidhihirisha kama mtetezi wa haki za binadamu na demokrasia, lakini taasisi huru za kimataifa zinapochunguza utendaji wa majeshi yake au ya washirika wake, huzituhumu taasisi hizo hizo kuwa zisizo na uwezo wa kutoa maamuzi au kwamba zinatoa maamuzi kisiasa. Kitendo ambacho sio tu kinatilia shaka uhalali wa madai ya Marekani, bali pia kinatuma ujumbe wa wazi kwa jamii ya kimataifa kwamba sheria za kimataifa huzingatiwa na nchi hiyo pale tu zinapopendelea na kuheshimu maslahi ya Washington.

Wakati huo huo, tishio la moja kwa moja dhidi ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai lina madhara makubwa kwa utaratibu wa kisheria kimataifa, mahakama ambayo falsafa ya kuundwa kwake ni kuweka utaratibu usio na upendeleo katika kushughulikia jinai za kivita na ukiukaji wa haki za binadamu. Ni wazi kuwa nguvu kubwa inapotumia lugha ya vitisho badala ya ushirikiano wa kisheria, uhuru wa taasisi hii huwa chini ya mashinikizo ambapo nchi nyingine pia zinaweza kukataa ushirikiana nayo. Suala hilo linaweza kudhoofisha pakubwa mifumo ya sheria za kimataifa na hivyo kuhatarisha maslahi ya wahanga wa jinai za kivita na migogoro mbali duniani.
Tishio la hivi karibuni la Washington linaweza kuchukuliwa kama sehemu ya juhudi pana za nchi hii za kuziwekea mipaka taasisi za kimataifa, taasisi ambazo zimeamua kuchunguza zaidi utendaji wa nchi kubwa duniani kuliko ilivyokuwa katika miaka ya huko nyuma. Kwa kufungua kesi zinazohusiana na Marekani na washirika wake, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC imeonyesha kwamba ina nia ya kuzingatia zaidi misingi ya haki na uadilifu kimataifa. Pamoja na hayo tabia ya karibuni ya Marekani inaonyesha kuwa njia hii inakabiliwa na vizingiti vikubwa.
Katika hali hiyo, umuhimu wa kusimama na kutetea taasisi za kimataifa unadhihirika wazi zaidi hivi sasa kuliko huko nyuma. Mahakama ya ICC, ingawa inakabiliwa na mashinikizo kutoka kwa nchi kubwa, falsafa yake imejikita katika misingi ya uhuru, kutopendelea upande wowote na kupigania haki za wanaodhulumiwa. Kuendeleza njia ya uchunguzi, hasa katika kesi nyeti na za gharama kubwa za kisiasa, ni mtihani mgumu kwa taasisi hii na kiwango cha kufungamana jamii ya kimataifa na misingi ya sheria za kimataifa. Ni kwa kusimama imara mbele ya mashinikizo na kuendeleza mchakato usio na upendeleo kwa upande wowote, tu, ndipo tunaweza kuwa na matumaini ya kupatikana haki kwa wahasiriwa wa vita na ukiukaji wa haki za binadamu na hivyo kudumisha imani ya jamii ya kimataifa kwa mifumo ya kimataifa.