Dar es Salaam. Mapinduzi ya teknolojia ya Akili Unde (AI) yanaendelea kubadilisha kwa kasi tasnia ya muziki duniani, hususan eneo la utengenezaji na utayarishaji wa muziki pamoja na video zake.
Kwa sasa, wataalamu na watayarishaji wa muziki duniani wanatumia zana mbalimbali zinazotumia AI, zikiwemo Suno AI inayotumika kuzalisha nyimbo kamili zenye sauti, midundo na maneno.
Pia, zana ya Udio inayotengeneza nyimbo kwa ubora wa juu wa sauti, ikizingatia mitindo mbalimbali ya muziki. Inasifika kwa uwezo wake wa kuunda nyimbo zenye muundo unaofanana na kazi za kibinadamu.
Nyingine ni AIVA, Amper Music, Soundraw, Boomy, LANDR na iZotope kwa ujumla
Zana hizi hutumiwa na wahandisi wa sauti kwa kazi za mastering, mixing na kuboresha ubora wa sauti kwa kutumia algorithimu za AI.
Pia zipo zana zinazoweza kuzalisha video za muziki kama vile Runway (Gen-2 / Gen-3), Pika Labs, Kaiber AI, Wonder Studio, Rotor Videos, Veed.io, Synthesia, zana zote hizo hutengeneza video zenye wahusika wa AI wanaoimba au kuzungumza.
Faida yake zana hizo hasa kwa wasanii wa Tanzania zina gharama ndogo za kutengeneza sauti na video, kasi kubwa ya uzalishaji, uhuru wa ubunifu pamoja na uwezo wa kushindana kimataifa kidijitali.
Kwa sasa kuanzia uandishi wa melodi, upangaji wa midundo, urekebishaji wa sauti hadi utoaji wa kazi kamili ya muziki, AI sasa ina uwezo wa kufanya majukumu ambayo kwa miongo mingi yalihitaji ubunifu wa moja kwa moja wa binadamu.
Hata hivyo, kwa upande chanya, AI imefungua milango kwa kizazi kipya cha wasanii na watayarishaji wa muziki, hususan wale wenye rasilimali ndogo. Programu zinazotumia AI zinaweza kutengeneza midundo, kusafisha sauti, au hata kuiga ala mbalimbali bila hitaji la studio ghali.
Hii itapunguza gharama za uzalishaji na kurahisisha mchakato wa kuingia sokoni. AI imeongeza kasi ya ubunifu pale watayarishaji wanatumia mifumo hii kama msaidizi wa kiubunifu inayopendekeza miundo ya nyimbo, mabadiliko ya sauti au mitindo mipya inayochanganya tamaduni tofauti.
Matokeo yake ni kuzaliwa kwa ladha mpya za muziki zinazovuka mipaka ya kijiografia na kijamii. Kwa kampuni za muziki, AI imekuwa nyenzo muhimu ya kibiashara. Kupitia uchambuzi wa data, teknolojia hii inasaidia kubaini ladha za wasikilizaji, kutabiri nyimbo zitakazopendwa na kupanga mikakati ya soko kwa ufanisi zaidi.
Hata hivyo, pamoja na fursa lukuki inazoleta, teknolojia hii pia imeibua mjadala mpana kuhusu mustakabali wa wasanii, haki miliki na uhalisia wa sanaa ya muziki.
Wanachosema watayarishaji wa Tanzania
Akizungumza na Mwananchi Matayarishaji mkongwe wa muziki nchini Tanzania Joachim Marunda ‘Master J’, anasema maisha yanabadilika hivyo ujio wa AI utatafsiriwa kama kitu kibaya kwa wale ambao hawakujiandaa lakini ni fursa kwa ambao walijiandaa kubadilika.
“Lazima tuangalie soko linaenda wapi kwa hiyo teknolojia hiyo itafanya watu wengi waumie lakini kwa wale watakaoipokea na kubadilika watapata fursa ya kutengeneza pesa,” amesema Master J.
Anasema nyimbo za AI ni nzuri na yeye amepata fursa ya kusikilizwa akisema ni teknolojia bora na ni ngumu kushindana nayo.
“Kwa kweli kwa watu watakaokuwa wanapata pesa ni wale watakaokuwa wataalamu wa kuitumia watu kama wasanii, watayarishaji na watunga mashairi wasipobadilika wataumia,” amesema.
Amesema rai yake kwanza kwa upande wa muziki AI imeshaingia kwahiyo waliopo kwenye muziki kwa sasa hawana budi kukubaliana nayo muhimu kukubali kubadilika.
Mtayarishaji wa muziki Ommy Dady Tz kutoka Studio ya MV09records, anasema kwake ni fursa japokuwa itakosa ubunifu wa binadamu.
Anasema katika miaka kumi ijayo kiwanda cha muziki kitakuwa na changamoto endapo kutakuwa na uzalishaji wa muziki ulioegemea teknolojia hiyo ya AI.
“Sio lazima kutumia AI hata huko mbeleni ubunifu wa kibinadamu lazima utahitajika hata kutakaposhamiri. Kwa Mfano mimi huwezi kuniambia nitumie AI au hata wasanii wakubwa wa huko mamtoni watumie AI. Kwa hiyo nafasi ya kibinadamu bado inahitajika na ni muhimu,” amesema.
Naye muongozaji video Deo Abel amesema bado kazi za AI haziwezi kuwa na ubora wa zile zinazotengenezwa na binadamu.
“AI haiwezi kuua ajira imekuja kutoa nafasi mpya na ajira mpya. Teknolojia mpya zinavyoingia zinaonekana kama tishio ni kama kwenye kompyuta watu walidhani wanapoteza ajira. Vitu ambavyo vitapungua ni kazi za kila siku.
“Kwenye production itaogeza ufanisi wa kazi na ajira kwa vijana ambao watajifunza kuitumia. Sidhani kama itaweza kuchukua ubora wa video zitazotengenezwa na binadamu kwa sababu inaweza kuwa na picha nzuri lakini haiwezi kubeba uhalisia au maumivu ambayo binadamu anaweza kuweka, “amesema Deon a kuongezea,
“Filamu ni zaidi ya picha kwa hiyo AI ni chombo tu lakini haiwezi kuweka uhalisia. Watu wajifunze mapema matumizi ya AI kwa sababu inaweza kuboost na kutengeneza ubora. Tuitumie kama msaidizi sio ifanye kila,”amesema
Kwa upande wake mzalishaji wa tamthilia ya Kombolela Abdul Juma, amesema ni kitu kizuri kwani itaibua vipaji vya watu
“Baadhi ya vijana ambao wamelowea humo katika kuandaa upande wetu wa filamu msanii atalipwa lakini sio kiasi kikubwa atapata hela kwa sababu itatumiwa picha yake lakini sio pesa nyingi kama sasa. Pia itarahisisha namna ya kuendesha budget kwetu maana hakutakuwa na watu wengi.
“ Lakini kitu tunachoweza kukimbilia kwa sasa kwani ubora wake bado haujafikia viwango. Watu itakuwa ngumu kuvumilia mapungufu. Mimi bado moyo wangu upo kwenye vitu halisi pale itapotengemaa nitajaribu lakini siwezi kusema nitaikimbia teknolojia,”amesema Abdul.
Ikumbukwe, pamoja na faida zake vilevile athari hasi za AI katika utengenezaji wa muziki haziwezi kupuuzwa. Moja ya hofu kubwa ni kupotea kwa ajira.
Wahandisi wa sauti, wapangaji wa midundo na hata wanamuziki wa ala halisi watakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa mifumo ya AI inayofanya kazi haraka na kwa gharama ndogo.
Hali hii imezua wasiwasi kuwa muziki unaweza kugeuka kuwa bidhaa ya “viwandani” inayozalishwa kwa wingi bila hisia wala uzoefu wa kibinadamu.
Wakosoaji wanasema AI haiwezi kuiga kikamilifu maumivu, furaha na simulizi binafsi ambazo kwa muda mrefu zimekuwa moyo wa muziki.
Changamoto za hakimiliki na maadili
Changamoto nyingine ni haki miliki. AI nyingi hufunzwa kwa kutumia mamilioni ya nyimbo zilizopo, mara nyingine bila idhini ya wasanii husika. Hili limeibua maswali nani anamiliki muziki uliotengenezwa na AI? Je, ni msanii, mtengenezaji wa programu au kampuni inayomiliki mfumo huo?
Pia kumekuwepo na matumizi ya AI kuiga sauti za wasanii maarufu bila ridhaa yao, hali inayotishia mapato yao na taswira zao binafsi.
Baadhi ya nchi zimeanza kujadili au kuweka sheria za kudhibiti matumizi haya, lakini kasi ya teknolojia inaonekana kuzidi utungaji wa sera.
Mustakabali wa muziki ni upi
Wataalamu wengi wanaona suluhisho si kupinga AI, bali kuisimamia kwa busara. Wanapendekeza mifumo ya kisheria itakayolinda haki za wasanii, sambamba na kuhimiza matumizi ya AI kama nyenzo ya kusaidia ubunifu wa binadamu, si kuubadilisha kabisa.
Kwa mtazamo huo, AI inaweza kuwa mshirika muhimu katika kuendeleza muziki wa dunia ikiwa itaendeshwa kwa uwazi, haki na maadili. Vinginevyo, kuna hatari ya soko la muziki kupoteza uhalisia wake na kugeuka kuwa tasnia inayoongozwa zaidi na algorithimu kuliko hisia za binadamu.
Wasanii waliotumia AI kwenye kazi zao
Kwa mara ya kwanza Bongo video rasmi ya wimbo wa Nandy, Sweety (2025) ambao ameshirikiana na Jux, ulitengenezwa kwa AI.
Video hiyo ilitengenezwa na AI9ja Studios kwa gharama ya Dola 4,500, wastani wa Sh11 milioni. Akizungumzia mradi huo, Nandy alisema baada ya kutoa video ya awali (visualizer) ya wimbo huo na ikafanya vizuri, aliona kuna sababu ya kuja na kitu cha tofauti ambacho kitaonyesha ubunifu.
“Nikasema tutarudi na video gani ambayo itafanya tuonekane tumefanya kitu cha maana au video itakayomfanya mtu apate stori ya kuiongelea. Nikafikiria mimi na Jux tuigize uhalisi ni kitu hakiwezekani, sisi ni wanandoa lazima tuheshimu ndoa.
“Kutokana na nafuatilia vitu, nikasema AI ni kitu kizuri sana kama tukipata mtu ambaye atafanya katika ubora na stori ikawa nzuri. Nikafikiri itakuwa ni kitu kizuri na sisi tutakuwa watu wa kwanza kufanya hivyo,” alisema.
Kwa upande wa Giggy Money ambaye ni kati ya wanaotumia teknolojia hiyo anasema.
“Inanirahisishia sana namtumia tu mtu atengeneze mimi nafanya kazi zangu nampeleka shule mtoto na umeona namna watu walivyovutiwa nao wakaanza kuiga nimefurahi,” alisema Gigy Money.