Mara. Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA) imetoa wito kwa Watanzania kuwekeza mkoani mara ili kukuza uchumi wa taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka hiyo, Balozi Dk Aziz Mlima, aliyewasili mkoani hapo mwishoni mwa juma.
Dk Mlima amesema mkoani hapo zipo fursa za uwekezaji ikiwemo uwepo wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, madini, pamoja na uvuvi hivyo Watanzania wachangamkie fursa hizo.
Wito huo unakuja ikiwa ni muendelezo wa kampeni ya uhamasishaji wa uwekezaji wa ndani yenye lengo la kutoa elimu na kuhamasisha Watanzania kushiriki kikamilifu katika uwekezaji kwa lengo la kukuza uchumi wa taifa.
“Katika kampeni hii tunatoa elimu kwa Watanzania ili waweze kuelewa fursa za uwekezaji zilizopo nchini hususani katika Mkoa wa Mara kwa kunadi fursa.
“Pia, na kuwahamasisha Watanzania kutumia fursa za uwekezaji zilizopo mkoani hapa, hususan katika sekta ya utalii kutokana na uwepo wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.” amesema.
Ameongeza kuwa Mkoa wa Mara ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa kuwa na akiba kubwa ya madini ya dhahabu, hali inayofungua wigo mpana wa uwekezaji katika sekta ya madini.
Aidha, amebainisha fursa nyingine muhimu zinapatikana katika ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba, kutokana na uwepo wa Ziwa Victoria, akisisitiza umuhimu wa Watanzania kuchangamkia fursa hizo.
“Tukiwa hapa Mkoa wa Mara tunatarajia kufanya kongomano la Uwekezaji wa Ndani Januari 26 pamoja na kutembelea miradi inayomilikiwa ma watanzania kwa kuona maendeleo ya miradi na kusikia shuhuda kwa watanzania hawa waliothubutu katika miradi ya uwekezaji hapa Mkoa wa Mara.”
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Emmanuel Mazengo, aliupokea ugeni wa TISEZA na kuipongeza kwa jitihada zake za kuhamasisha uwekezaji wa ndani, akisisitiza ushirikiano kati ya Mkoa wa Mara na mamlaka hiyo katika kukuza uchumi wa wananchi.