Waziri wa Ulinzi wa Venezuela amethibitisha kwamba Marekani ilitumia silaha zisizojulikana wakati wa shambulizi la kumteka nyara Rais Nicolas Maduro wa nchi hiyo.

Jenerali Vladimir Padrino López amesema kwamba jeshi la Marekani lilitumia silaha ambazo hazijawahi kutumika kwenye uwanja wa vita wakati wa operesheni ya kumkamata rais wa Venezuela mjini Caracas.

“Katika eneo hili tunakosimama sasa, uvamizi wa kijeshi ulifanywa na nguvu kubwa na hatari zaidi ya nyuklia duniani,” amesema Jenerali Padirino Lopez akiuambia mkusanyiko wa wanajeshi wa Venezuela.

Lopez amekumbusha kwamba Rais wa Marekani, Donald Trump alisema waziwazi siku mbili zilizopita wakati wa mkutano wa kila mwaka wa Jukwaa la Uchumi Duniani huko Davos kwamba Marekani ilitumia silaha mpya ambazo hazijawahi kufanyiwa majaribio katika kutekeleza operesheni ya kumteka nyara Maduro.

Waziri wa Ulinzi wa Venezuela ameongeza kuwa, silaha zilizotumiwa na Marekani dhidi ya watu wa Venezuela zimeigeuza nchi hiyo kuwa “maabara ya silaha za Marekani.”

Tarehe 3 mwezi huu wa Januari, Marekani iliivamia Venezuela na kumteka nyara Rais wa nchi hiyo, Nicolas Maduro na mkewe, Cilia Flores.

Siku chache baada ya hujuma hiyo iliyokiuka sheria za kimataifa, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Venezuela alisema idadi ya watu waliouawa na kujeruhiwa katika shambulio la Marekani ilipindukia watu 200.

Alisema, “Shambulio hilo lilikuwa la kuogofya. Ni ukweli mchungu ambao hauwezi kufichika. Hata wanawake waliokuwa katika majumba yao walishambuliwa na kujeruhiwa wakati wa hujuma hiyo ya kivamizi ya Januari 3.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *