
Wakati Asnath Yusuph aliporejea shuleni Bagamoyo, hakuwa anarudi kwenye masomo pekee; alikuwa akirejesha matumaini ya maisha ambayo yalikuwa karibu kupotea. Ujauzito ulimlazimu kuacha masomo ya sekondari akiwa Kidato cha Pili, hali ambayo wasichana wengi huiishi kama mwisho wa safari yao ya kielimu. Kwa muda mrefu, aliamini kuwa shule haikuwa tena sehemu ya maisha yake.
“Baada ya kupata ujauzito, nilikata tamaa kabisa ya kuendelea na masomo,” anakumbuka. “Lakini niliposikia kuna fursa ya kurejea shuleni, niliamua kujaribu tena. Sasa nimerudi darasani kama wanafunzi wengine, na nina ndoto ya kuwa mhasibu.”
Tanzania inapoadhimisha Siku ya Kimataifa ya Elimu 2026 chini ya kaulimbiu ya kimataifa “Nguvu ya Vijana katika Ushirikiano wa Kuboresha Elimu”, simulizi ya Asnath inaakisi uhalisia mpana wa kitaifa. Inaangazia mamilioni ya vijana ambao masomo yao yamekatizwa na umaskini, mila na desturi, jiografia au mazingira ya maisha, pamoja na ongezeko la uelewa kuwa mifumo ya elimu inapaswa kujibadilisha kulingana na mahitaji ya wanafunzi na si vinginevyo.
Lengo la Maendeleo Endelevu namba 4 (Elimu Bora) linaungwa mkono na serikali, ila pia taasisi mbalimbali, ikiwemo Stromme Foundation, ambayo inaendeleza elimu jumuishi, yenye usawa na ubora kupitia mipango bunifu ya kujifunza inayotegemea jamii, inayowawezesha vijana na kupanua fursa za elimu nchini Tanzania. Jitihada hizi zinaendana pia na dira ya muda mrefu ya maendeleo ya taifa, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayoweka rasilimali watu kuwa kiini cha mabadiliko ya taifa. Dira hiyo inatambua kuwa elimu bora na jumuishi si huduma ya kijamii pekee, bali ni msingi wa ukuaji wa uchumi, mshikamano wa kijamii na ustahimilivu wa taifa. Msingi huu unaimarishwa zaidi na Sera ya Elimu na Mafunzo, inayothibitisha haki ya kila mwanafunzi wakiwemo vijana walioko nje ya mfumo rasmi wa shule kupata njia mbadala na jumuishi za elimu.
Katika jamii mbalimbali, dhamira ya sera hizi inaanza kuonekana kupitia mifumo ya elimu ya fursa ya pili na vituo mbadala vya kujifunzia vinavyoungwa mkono na ushirikiano kati ya asasi za kiraia, jamii Pamoja na serikali. Stromme Foundation, kushirikiana na mashirika ya ndani kama Shirika la Maendeleo ya Jamii (OCODE) yamesaidia vijana kama Asnath kurejea masomoni, huku pia yakiwapa vijana wasioweza kurudi katika mfumo rasmi mafunzo ya stadi za maisha na ufundi yanayowaandaa kwa ajira au kujitegemea. Jitihada hizi zinaongozwa na ushauri wa kitaalamu (mentorship), ushiriki wa wazazi, na ushirikiano wa karibu na maafisa elimu katika ngazi ya jamii.
“Kilicho na maana kubwa katika kazi yetu ni kuona mabadiliko halisi ndani ya jamii,” anasema Tunu Sanga, Afisa Programu Elimu wa OCODE. “Msichana anaporudi shuleni au kijana anapoanzisha biashara yake mwenyewe, hilo linaakisi dhamira ya pamoja na ushirikiano imara.”
Kinachozitofautisha mbinu hizi si tu kutoa fursa ya kuingia darasani, bali pia namna elimu yenyewe inavyoundwa. Katika mazingira ya elimu mbadala, wanafunzi hushiriki kikamilifu katika majadiliano, kujifunza kwa wenzao, na kufikiri kwa kina, wakichangia kuunda maudhui ya masomo kulingana na uzoefu wao wa maisha na ndoto zao. Elimu inakuwa mchakato wa pamoja unaojengwa na wanafunzi, walimu, wazazi na jamii kwa ujumla.
Matokeo yake yanaonekana wazi. Katika Shule ya Msingi Nia Njema, Bagamoyo, idadi ya wanafunzi wanaojiunga na madarasa ya elimu mbadala imeongezeka zaidi ya mara mbili kwa kipindi kifupi.
“Tulipoanza, tulikuwa na watoto 65, wengi wao hawakuhudhuria shule mara kwa mara,” anaeleza Mwalimu Mwanahamisi Msagati, mwalimu wa MEMKWA. “Leo hii, tuna watoto 137 wanaohudhuria masomo kila siku.”
Hata hivyo, mafanikio haya pia yanaibua changamoto zinazoendelea. “Darasa sasa ni dogo na lipo katika hali isiyoridhisha,” anaongeza. “Bado tunahitaji vifaa zaidi vya kujifunzia na mwalimu wa ziada, kwa kuwa mahitaji yanaendelea kuongezeka.”
Shinikizo hili linaashiria changamoto ya kitaifa: pale elimu jumuishi inapofanikiwa, lazima iandamane na uwekezaji endelevu katika miundombinu, walimu na rasilimali za kujifunzia.
Kwa kuwahusisha wazazi na walezi katika Vikundi vya Akiba na Mikopo vya Jamii (CMSG), jitihada hizi zinaimarisha uendelevu na kuhakikisha watoto wanaendelea kuungwa mkono kielimu hata baada ya miradi kumalizika.
Simulizi ya elimu shirikishi inaanza mapema zaidi katika elimu ya awali. Vituo vya Malezi, Makuzi na Elimu ya Awali ya Mtoto (ECCE) vinawasaidia watoto kuanza shule ya msingi wakiwa na kujiamini na utayari wa kujifunza. Katika Shule ya Msingi Mswakini Juu, walimu wanaona tofauti kubwa.
“Darasa la Kwanza lina watoto wengi waliotoka Kituo cha Randilen,” anasema Charles Mwenda, mwalimu wa shule ya msingi Mswakini juu Wilaya ya Monduli. “Watoto hawa huja tayari wanajua kusoma, kuandika na kuhesabu.”
Kituo cha Randilen ni miongoni mwa jitihada kadhaa za kijamii zinazoungwa mkono kupitia ushirikiano kati ya Stromme Foundation na Maasai Pastoralist Development Initiative (MPDI) mkoani Arusha. Hata hivyo, umbali mrefu wa shule za umma katika maeneo ya vijijini na ya wafugaji bado ni kikwazo kwa watoto kupata elimu ya awali, hali inayodhihirisha umuhimu wa msaada zaidi wa serikali katika kupeleka huduma za ECCE karibu na jamii.
Kwa pamoja, uzoefu huu unaonesha mabadiliko ya kimyakimya lakini yenye nguvu kuhusu namna elimu inavyoeleweka. Maafisa elimu, walimu, wazazi, mashirika ya kiraia, serikali, na vijana wenyewe wanafanya kazi kwa pamoja kujenga mifumo ya elimu inayoakisi mahitaji ya watu, inayowajibika, na yenye utu.
Tanzania inapoelekea mwaka 2050, swali si tena kama vijana wanapaswa kushiriki katika kuunda elimu, bali ni kama mifumo ya elimu iko tayari kukubali kikamilifu mchango wao kama washirika wa ujenzi wa elimu. Sauti zinazotoka katika madarasa, vituo vya elimu ya awali na mazingira ya elimu mbadala zinatoa jibu wazi: vijana wanapoaminiwa na kuungwa mkono, elimu inakuwa jumuishi zaidi, yenye maana zaidi, na yenye kuleta mabadiliko ya kweli.
Mwaka huu, Stromme Foundation inaadhimisha miaka 50 tangu ilipoanzishwa na miaka 22 ya utekelezaji nchini Tanzania. Hadi sasa, Stromme Foundation imefikia shule za umma 14, zimeimarisha uwezo wa walimu zaidi ya 200, na kuwafikia zaidi ya wanafunzi 15,000 zikichangia kujengwa kwa mifumo ya elimu jumuishi na inayojali mahitaji ya jamii.
“Stromme Foundation Tanzania inaendelea kuwa na dhamira ya dhati ya kuunga mkono maendeleo ya Tanzania kupitia uwezeshaji wa vijana. Tutaendelea kuimarisha ushirikiano wetu na Serikali ili kuhakikisha jitihada zetu zinachangia kikamilifu katika kasi ya kitaifa ya kufikia Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050,” alisema Alunas Mwamakimbula, Meneja wa Programu wa Stromme Foundation Tanzania.
Vijana hawasubiri kuwezeshwa tayari wanafanya kazi. Mifumo ya elimu inapotoa nafasi ya sauti zao, hairejeshi tu fursa za kujifunza, bali pia hujenga mustakabali ulio na usawa, ustahimilivu, na unaomilikiwa kwa pamoja.