Tangazo la Marekani la kuunda Bodi ya Amani ya Gaza limeibua wasiwasi mkubwa kuhusu jaribio la Trump la kudhoofisha Umoja wa Mataifa, sambamba na kupeleka mbele ajenda yake binafsi ya kupenda jaha na kujipanua kisiasa.
Chombo hicho kipya cha kimataifa ambacho kilipendekezwa na Rais wa Marekani, Donald Trump, ili kuendeleza mpango wa amani wa Gaza, ingawa mwanzoni kiliungwa mkono wa Umoja wa Mataifa, lakini sasa kimeibua wasiwasi mkubwa kadiri maelezo yake yanavyozidi kuwa wazi. Bodi hiyo, ambayo itaongozwa na Donald Trump maisha yake yote hata baada ya kumalizika kipindi chake cha urais, imepangwa kushughulikia migogoro mingine ya kimataifa katika hatua zijazo. Kwa hakika, Trump anaendeleza mpango wa “Bodi ya Amani” (Board of Peace), katika fremu ya malengo yake ya kupenda jaha ya kisiasa, ambao lengo lake sasa limebadilika kutoka kuwa chombo cha kushughulikia usitisha mapigano huko Gaza na kuwa taasisi ya upatanishi ya kimataifa. Muundo wa usimamizi wa bodi hiyo unajumuisha majina maarufu kama vile mkwe wa Trump, Jared Kushner, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio, na Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Tony Blair kama wanachama wa bodi ya utendaji. Hatua ya Trump ya kumteua Tony Blair katika “bodi ya utendaji ya waasisi” ya Board of Peace imeibua utata mkubwa.

Msimamo wa kisiasa wa nchi za dunia kuhusu chombo hicho umegawanyika katika makundi matatu: Kambi ya waliojiunga na bodi hiyo, nchi ambazo zimekataa kujiunga, na nchi ambazo bado zinasitasita katika suala hilo. Nchi nyingi zilizoafiki bodi hiyo ziko Asia Magharibi, Asia ya Kati, na maeneo ya Ulaya Mashariki. Saudi Arabia, UAE, Qatar, Misri, Uturuki, na Bahrain zimethibitisha kujiunga na bodi hiyo ya Trump. Pia, nchi kutoka Caucasus na Asia ya Kati, kama vile Jamhuri ya Azerbaijan, Armenia, Kazakhstan, Mongolia, na Uzbekistan, pamoja na Morocco, Paraguay, Argentina, Hungary, Belarusi, Pakistani na Vietnam ziko kwenye orodha ya wanachama wa bodi hiyo. Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu pia amekubali uanachama katika bodi hiyo, licha ya kukosoa uwepo wa Qatar na Uturuki katika chombo hicho. Trump pia amedai kwamba Rais wa Russia, Vladimir Putin amekubali kushiriki katika Bodi ya Amani na amejitolea kulipa ada ya uanachama ya dola bilioni 1 kutoka kwenye mali za Russia zinazozuiliwa nchini Marekani. Hata hivyo, Russia bado haijatangaza msimamo rasmi kuhusu suala hilo. Utofauti wa maeneo ya kijiografia ya wananchama wa bodi hiyo unaonyesha hamu ya Trump ya kujenga muungano mpana, zaidi ya washirika wa jadi wa Magharibi.
Kwa upande mwingine, nchi kadhaa za Ulaya zimepinga waziwazi mpango huo au kwa uchche, zimekataa kujiunga nao kwa sasa. Uingereza, Ufaransa, Sweden, Norway na Slovenia ni miongoni mwa nchi ambazo zimekataa mwaliko wa Trump. Wapinzani wa Magharibi wa mpango huo wamekataa mwaliko huo, wakipinga uwezekano wa Russia kuwepo kwenye chombo hicho na utata kuhusu mwingiliano wa chombo hicho na kazi za Umoja wa Mataifa. Idadi kubwa ya nchi bado hazijatangaza msimamo wao wa mwisho. Miongoni mwao, kuna nchi muhimu kama vile China, Russia, India na Ujerumani. Tume ya Ulaya na nchi kama vile Ukraine, Italia na Singapore pia bado zinachunguza hali ya mambo. Msimamo wa nchi hizi unaonyesha ugumu wa kidiplomasia na utata kuhusu mamlaka ya Bodi ya Amani na malengo yake ya mwisho.
Trump amedai kwamba chombo hicho kitachukua “mbinu ya ujasiri na mpya ya kutatua migogoro ya kimataifa.” Hii imetafsiriwa na baadhi kama hatua ambayo inaweza kudhoofisha msimamo wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambalo kwa sasa lina jukumu la kuweka na kudumisha amani na usalama wa kimataifa.
Kimsingi, Bodi ya Amani ya Gaza, ambayo Donald Trump ameianzisha inatambuliwa na nchi nyingi na wachambuzi wa mambo kama jaribio la kudhoofisha Umoja wa Mataifa. Sababu kuu ya mtazamo huu ni kwamba, kinyume na madai ya awali ya kujikita kwenye suala la Gaza, chombo hiki kimekuwa taasisi pana yenye mamlaka ya juu ya mataifa, na sasa kinaingia katika maeneo ambayo, kwa mujibu wa muundo wa sheria za kimataifa, yako chini ya mamlaka ya Umoja wa Mataifa. Mbali na hayo, wakati wa uzinduzi wa bodi hiyo, Trump mwenyewe alitangaza kwamba chombo hicho kinaweza “kufanya karibu chochote kinachotaka,” hata kupanua kazi zake hadi kwenye migogoro mingine ya kimataifa, jukumu ambalo kwa kawaida ni la Umoja wa Mataifa.
Wakosoaji wa Ulaya na kimataifa wameonya kwamba mpango huo unaweza kudhoofisha utaratibu uliopo wa kambi kadhaa kwa kuunda muundo sambamba. Baadhi ya nchi, ikiwa ni pamoja na Ufaransa, zimekataa kujiunga na chombo hicho, zikihofia kwamba kitakiuka kanuni za Umoja wa Mataifa na kutishia kuchukua nafasi ya taasisi hiyo. Ripoti kutoka Ujerumani pia zinaonyesha kwamba maafisa wa nchi hiyo wana wasiwasi kwamba chombo hicho kinaweza kuwa “msumari wa mwisho katika jeneza la sheria za kimataifa”, kwa sababu kitakwepa mifumo ya Umoja wa Mataifa na kuweka maamuzi ya kimataifa kwenye udhibiti wa mtu binafsi, chini ya ushawishi wa Marekani.
Kioja zaidi ni kwamba, Donald Trump amejitangaza kuwa rais wa maisha wa chombo hicho na ameweka ada ya dola bilioni 1 kwa ajili ya kupata uanachama wa kudumu kwenye chombo hicho, hatua ambayo wengi wanaona kuwa inapingana na kanuni za uwazi, kutopendelea upande wowote na usawa ambazo ndio msingi wa Umoja wa Mataifa.