
Mapigano mapya nchini Sudan Kusini yamewalazimisha watu zaidi ya 180,000 kuyahama makazi yao, huku mashuhuda wakizungumzia utumiaji holela wa mabomu ya mapipa na raia kukimbilia kwenye vinamasi, huku hali tete ya ukosefu wa amani ikitanda nchini humo.
Sudan Kusini, nchi changa zaidi duniani, imekumbwa na vita, umaskini na ufisadi mkubwa tangu ilipoundwa mwaka 2011. Ghasia zimeongezeka tena nchini humo kati ya makundi hasimu ambayo kwa sasa yamejielekeza katika jimbo la Jonglei, kaskazini mwa mji mkuu, Juba.
Daniel Deng mwenye umri wa miaka 25 raia wa Sudan Kusini aliyelazimika kuhama makazi yake anasema: “Nimekwama na hali ya mambo inaendelea kuvurugika; sehemu pekee salama ya kukimbilia ni kwenye vinamasi.”
Deng ametoa mfano wa mapigano makali wiki jana katika Kaunti ya Duk anapoishi baada ya makundi hasimu kudhibiti eneo hilo na kisha kufurushwa na jeshi la Sudan Kusini. Amesema karibu wapiganaji 300 waliuliwa katika mapigano hayo.
Mkataba wa kugawana madaraka kati ya pande mbili kuu, yaani serikali ya Juba na upinzani, umekufa baada ya Rais Salva Kiir kupingana na makamu wake , Riek Machar, ambaye alikamatwa Machi mwaka jana; na sasa anakabiliwa na kesi ya “uhalifu dhidi ya binadamu”.
Mamlaka za Sudan Kusini zinakadiria kuwa idadi ya watu waliolazimika kuhama makazi yao ni zaidi ya 180,000 katika kaunti nne za Jonglei.
Kiir na Machar walipigana vita vya miaka mitano muda mfupi baada ya Sudan Kusini kupata uhuru; vita ambavyo vimegharimu maisha ya watu 400,000. Makubaliano ya kugawana madaraka yaliyofikiwa mwaka 2018 yalidumisha amani kwa miaka kadhaa; hata hivyo mipango ya kuitisha uchaguzi na kuunganisha majeshi yamegonga mwamba.