Kadiri wimbi la fitina, vurugu na machafuko yanayohusishwa na ushawishi wa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel nchini Iran lilivyozidi kupamba moto, nafasi ya vyombo vya habari hasimu katika kuchochea vitendo vya ugaidi na kukiuka wazi misingi ya sheria za kimataifa imejitokeza kwa uwazi tena.
Katika machafuko ya hivi karibuni nchini Iran, vyombo vya habari hasimu na vinavyopinga Mapinduzi ya Kiislamu, hasa kituo cha televisheni kinachojiita Iran International, ambacho ni nguzo kuu ya propaganda za Magharibi dhidi ya Iran, vimekuwa vikizalisha na kusambaza taarifa maalumu za upotoshaji.
Vyombo hivi vya habari vimekuwa vikichochea hali ya wasiwasi wa kisaikolojia, kueneza hisia za kukata tamaa, na kutoa mwanya wa kuungwa mkono kwa makundi yanayotumia mabavu na ya kigaidi. Uchochezi huu wa ugaidi unaweza kutathminiwa kuwa ni ukiukaji wa sheria na makubaliano ya kimataifa yanayohusiana na mapambano dhidi ya ugaidi.
Vyombo hivi vya habari, ikiwemo Iran International, BBC Persian na baadhi ya mitandao mingine, havifanyi kazi ndani ya mipaka ya uandishi wa habari wa kitaalamu, bali vimejihusisha na kile kinachoweza kutafsiriwa kama “vita vya kisaikolojia”, “operesheni za kijasusi”, na “uungaji mkono wa kimaudhui kwa vitendo vinavyohusishwa na ugaidi”.
Kwa sasa, kuna takribani mikataba na makubaliano karibu 20 ya kikanda na kimataifa yanayohusu mapambano dhidi ya ugaidi wa kimataifa. Nchini Uingereza, taasisi inayojulikana kama Ofcom ndiyo yenye dhamana ya kusimamia kanuni za utangazaji, mawasiliano ya redio, na uangalizi wa shughuli za vituo vya redio na televisheni. Kila kituo cha televisheni kinachotaka kufanya kazi ndani ya nchi hiyo kinapaswa kupata leseni kutoka Ofcom, na iwapo masharti ya leseni yatakiukwa, kituo husika kinaweza kukabiliwa na kufutiwa leseni na kusimamishwa shughuli zake.
Mji mkuu wa Uingereza, London, ni makao ya kituo cha televisheni kinachojiita Iran International, sambamba na BBC Persian na baadhi ya televisheni nyingine zinazo chochea ugaidi. Kwa kuunga mkono ugaidi waziwazi kupitia mahojiano na vipindi vyao, pamoja na kutangaza kwa uwazi misimamo ya makundi hayo ya kigaidi, vituo hivyo vimekiuka bayana kanuni za Ofcom.
Mashirika haya ya habari, ambayo hudai kuwa yanatangaza kwa ajili ya wazungumzaji wa lugha ya Kifarsi, hulenga kutekeleza operesheni za kisaikolojia, kusambaza taarifa potofu, kuunda mazingira ya hofu na kukata tamaa katika jamii, pamoja na kutoa majukwaa ya kimitandao kwa makundi na mashirika ya kigaidi na kuchochea matumizi ya vurugu.
Kwa kuzingatia machafuko na vitendo vinavyofanana na ukatili wa makundi ya kigaidi kama Daesh (ISIS) dhidi ya raia wa kawaida nchini Iran, inaonekana kwamba aina zote za ukiukaji wa makubaliano na sheria za kimataifa zimejitokeza kupitia shughuli za mashirika hayo ya utangazaji yanayohusishwa na Marekani na Israel.
Kwa mujibu wa sheria za kimataifa, iwapo itathibitika kwamba chombo cha habari kimetoa taarifa za uongo kwa makusudi na kitendo hicho kikasababisha moja kwa moja vitendo vya vurugu, ugaidi au kuhatarisha usalama wa umma, basi chombo hicho kinaweza kuwajibishwa kisheria.

Baadhi ya vyombo vinavyojiita vya habari kwa lugha ya Kifarsi vinavyoendesha shughuli zao nje ya Iran—hasa televisheni inayojiita Iran International na BBC ya lugha ya Kifarsi—vimekuwa na nafasi iliyoratibiwa na yenye uzito katika kuchochea vurugu, kuonyesha uungaji mkono kwa makundi yanayoelezwa kuwa ya kigaidi, na kutekeleza operesheni za kisaikolojia dhidi ya usalama wa taifa la Iran. Shughuli zao dhidi ya usalama wa wananchi wa Iran zinaweza kutathminiwa kupitia mihimili kadhaa mikuu kama ukiukaji wa sheria za kimataifa na kanuni za kitaaluma za utangazaji.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaamini kwamba baadhi ya vyombo vya habari vya Kifarsi vinavyoendesha shughuli zao nje ya nchi, kwa kufanya mahojiano na makundi yanayoelezwa kuwa ya kigaidi, kuonyesha taswira za vitendo vya vurugu, kuwakaribisha wasemaji wa makundi yanayotaka kujitenga, na kushabikia operesheni za kigaidi, vimekiuka wazi sheria za kimataifa pamoja na kanuni za kitaaluma za utangazaji.
Kwa mujibu wa Azimio namba 1373 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lililopitishwa mwaka 2001, nchi wanachama zinawajibika kuzuia aina yoyote ya msaada wa moja kwa moja au usio wa moja kwa moja kwa makundi yanayoelezwa kuwa ya kigaidi, na pia kuzuia shughuli zozote za kutangaza, kueneza au kutoa uhalali wa kisiasa kwa vitendo vya kigaidi.
Kwa mtazamo wa Iran, vyombo vya habari vinavyotoa jukwaa kwa makundi ya kigaidi na viongozi wao, pamoja na nchi zinazowapa hifadhi au kuunga mkono waendeshaji wa vyombo hivyo, ni mifano ya wazi ya uungaji mkono wa ugaidi.
Shughuli za baadhi ya vyombo vinavyoonekana kuwa vya uhasama haziendeshwi kwa mujibu wa kanuni za kitaaluma za utangazaji, bali zinaangukia katika mkondo wa hatua za chuki, vita vya kisaikolojia na uungaji mkono usio wa moja kwa moja kwa vitendo vya ugaidi. Vyombo hivi vinachukuliwa kuwa vinakiuka sheria za kimataifa za kupambana na ugaidi, kanuni za Ofcom, pamoja na misingi ya msingi ya sheria za kimataifa, na hivyo vinaweza kuwekwa katika kundi la “vyombo vya habari vya kigaidi”.