Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 zilifikia tamati Jumapili, Januari 18, 2026 ambapo Senegal iliibuka bingwa baada ya kuipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji Morocco.

Hata hivyo fainali hiyo iliingia doa katika dakika za majeruhi za muda wa kawaida wa mchezaji baada ya kundi kubwa la wachezaji na maofisa wa benchi la ufundi la Senegal wakiongozwa na Kocha Mkuu, Pape Thiaw kugoma kwa muda kabla ya baadaye kuamua kuendelea na mech.

Thiaw aliwaamuru wachezaji wake kutoka nje ya uwanja kufuatia uamuzi wa Refa Jean-Jacques Ndala kuamuru penalti kwenda langoni mwao baada ya Brahim Diaz kufanyiwa faulo na Malick Diouf.

Hata hivyo nyota wa Senegal, Sadio Mane alionekana kutokubaliana na uamuzi wa kuondoka uwanjani ambapo alionekana akiwashawishi wenzake kundelea na mchezo.

Uamuzi wa Senegal kurejea uwanjani na kuendelea na mchezo, ulikuwa na faida kwa upande wao kwani Morocco walikosa mkwaju huo wa penalti uliopigwa na Brahim Diaz na baadaye ikatwaa ubingwa kwa ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Pape Gueye.

Kwa misingi ya mchezo wa soka, kitendo kilichofanywa na Senegal kugomea uamuzi wa refa na mchezo kiujumla hakikuwa sahihi na kinatia doa taswira ya mchezo wa soka barani Afrika na pia kushusha thamani ya mashindano ya AFCON ambayo ndio yenye thamani na mvuto mkubwa zaidi barani humu.

Hata hivyo naamini ingewezekana mapema kuepuka kile kilichofanywa na Senegal katika mchezo ule iwapo baadhi ya mambo yangefanyiwa kazi na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ambalo ndio lenye mashindano hayo na ndio limekuwa likiyasimamia.

Kwa mtazamo wangu, hayo mambo nadhani ndio yalichangia kwa kiasi kikubwa kuishawishi Senegal ifanye tukio lile na iwapo yangeshughulikiwa mapema sidhani kama lililotokea tungeliona.

Miongoni mwa mambo hayo ni uchezeshaji ulioonekana una mlengo wa kunufaisha timu mwenyeji ambaye ni Morocco badala ya kutengeneza mazingira ya usawa kwa timu zote shiriki.

Kuanzia katika mechi ya hatua ya 16 bora hadi fainali, kuna matukio ambayo timu pinzani zilistahili kunufaika nayo kihalali lakini waamuzi hawakuamuru ipasavyo na zikashindwa kupata haki zilizostahili lakini yapo ambayo Morocco haikustahili kunufaika nayo na ikapata haki isiyostahili.

Hayo yote yalilalamikiwa lakini hakukuwa angalau hata na kauli kutoka CAF ya kujitenga na lawama hizo jambo ambalo lilifanya wengi wazidi kuwa na wasiwasi na hali ya mambo katika mashindano hayo.

Mfano katika hatua ya 16 bora, timu ya Taifa ya Tanzania ilistahili kupata penalti baada ya Iddi Selemani ‘Nado’ kuangushwa katika eneo la hatari lakini haikupata, ikatokea tena katika robo fainali ambapo Cameroon mchezaji wake alifanyiwa faulo katika boksi la Morocco lakini haikupata mkwaju wa penalti iliyostahili.

Katika hiyo fainali yenyewe dhidi ya Senegal, refa alifanya kosa la kuua shambulizi ambalo baadaye lilizaa bao lililokataliwa akidai kuwa mchezaji wa Morocco alifanyiwa faulo lakini picha za marejeo zilionyesha kwamba hakukuwa na faulo ambayo yeye aliitafsiri.

Ukiondoa uchezeshaji usioridhisha, yapo matukio mengi ya nje ya uwanja ambayo hayakuwa ya kiungwana yaliyofanywa na wenyeji lakini CAF haikuchukua hatua zozote wala kutoa kauli za kulaani.

Mfano ni timu ya Taifa ya Senegal kutopatiwa ulinzi wakati ilipokuwa ikielekea Rabat kwa ajili ya fainali lakini pia ililalamika kupangiwa kiwanja cha mazoezi katika eneo ambalo timu ya taifa ya Morocco iliweka kambi yake.

Ikumbukwe pia matukio kama usumbufu kwa makipa wa timu pinzani kutoka kwa waokota mipira na wachezaji wa Morocco ambao walikuwa wakichukua mataulo yao ambayo huyatumia kujifutia maji na jasho lakini hakuna hatua zilizokuwa zikichukuliwa.

Ukimya wa CAF katika kukemea yale yaliyoonekana kuwa kinyume na Morocco ulikuwa unatengeneza vinyongo ambavyo baadaye vingezalisha bomu kama lile la Senegal kugomea mchezo muhimu na mkubwa wa fainali.

Kimsingi kama CAF ingeshughulika na moshi, moto usingewaka. Kwa bahati mbaya iliacha moshi ufuke na sasa inahangaika kuzima moto.

Tujifunze kuchukua hatua pindi kunapoibuka malalamiko vinginevyo yale yaliyotokea katika fainali ya AFCON 2025 yanaweza kujirudia tena barani Afrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *