Marekani. Rapa kutokea Marekani, 50 Cent anajulikana kuwa si mtu wa kuogopa kuingilia mijadala yenye utata kwenye mitandao ya kijamii, lakini anasema kuna mijadala ya aina mbili ambayo amekuwa akijiepusha nayo.
50 Cent, mkali wa kibao cha Candy Shop (2005), ameitaja mijadala ya kidini na kisiasa kama mambo ambayo amekuwa akijizuia kujihusisha nayo katika mitandao maana anajua athari zake.
Akizungumza huko West Hollywood wakati wa uzinduzi wa Moses the Black, filamu ambayo yeye ni mmoja wa watayarishaji wake, alieleza kwanini filamu hiyo imejikita kwenye burudani badala ya masuala ya kidini.
“Kuna mambo mawili wanakuambia uyaepuke. Wanakuambia ukae mbali na dini na ukae mbali na siasa, kwa sababu haijalishi unaamini nini, kutakuwa na mtu anayepingana na wewe kwa hisia kali,” alisema.
Aliwataja baadhi ya wasanii wenzake kama Nicki Minaj na Ye (zamani Kanye West) kama mifano ya wasanii ambao wamekuwa wakizungumza waziwazi kuhusu dini na siasa ila baadaye wakajikuta katika wakati mgumu.
“Mimi najiepusha na mambo hayo. Hapo ndipo Kanye West alipoharibu mambo. Halafu Nicki Minaj naye akasema maneno fulani. Inaonekana kama ni wazimu, lakini huo ndio ukweli wenyewe,” alisema 50 Cent.
Ikumbukwe Nicki Minaj na Kanye West wote wamewahi kujikuta katikati ya mijadala mikubwa ya kisiasa na kidini miaka ya hivi karibuni, mijadala ambayo haikuwa na matokeo mazuri kwao.
Nicki amewahi kuzungumzia madai ya kuteswa kwa Wakristo nchini Nigeria na pia kupongeza utawala wa Rais Donald Trump, hatua iliyomfanya kukosolewa sana hadi kujiondoa katika mtandao wa Instagram.
Kwa upande wa Kanye West, alionyesha kumuunga mkono Trump na kumsifu mara kadhaa tangu kipindi chake cha kwanza cha Urais, na hata alijaribu kugombea urais wa Marekani mwaka 2020 lakini hakufanikiwa.
Mwaka 2022, Kanye West alitoa kauli nyingi za chuki dhidi ya Wayahudi, jambo lililosababisha kampuni kama Adidas, Balenciaga na Universal Music Group kusitisha ushirikiano naye wa kibiashara.
Kuhusu filamu ya Moses the Black ya 50 Cent, inatarajiwa kuanza kuonyeshwa kwenye kumbi za sinema hapo Januari 30, na pia inawahusisha wasanii wengine wa rap kama Wiz Khalifa na Quavo.
Utakumbuka jina la 50 Cent lilichomoza kimuziki mara baada ya kukutana na Eminem na Dr. Dre ambao walimsaidia kusaini mkataba na lebo ya Aftermath Entertainment iliyomtoa.
Albamu yake ya kwanza, Get Rich or Die Tryin’ (2003) ilipata mafanikio makubwa duniani ikitoa nyimbo kali ukiwemo In Da Club, na kumfanya kuwa mmoja wa wasanii wakubwa zaidi wa Hip Hop kwa wakati huo.
Pia alifanikiwa kuanzisha kundi la G-Unit, lililochangia kuibua wasanii wengine na kupanua ushawishi wake katika Hip Hop ya kimataifa.
Mbali na kuendelea kufanya muziki na show, amepata mafanikio makubwa katika biashara ya burudani hasa katika utayarishaji wa filamu na vipindi vya televisheni. Na sasa anatambulika kama mmoja wa magwiji wa Hip Hop wenye mafanikio kiuchumi.