Dar es Salaam. Unafahamu kuwa namba tano ina nafasi kubwa kwenye maisha ya nyota wa muziki nchini, Abigail Chams?
Mkali huyu wa vibao kama vile Mee Too , Closer, Leave Me Alone na msanii wa kwanza wa kike kutoka Afrika Mashariki kutajwa kuwania tuzo za BET 2025, anaitaja namba tano kuwa ya bahati kwake.
“Imekuwa ikimaanisha kila kitu katika maisha yangu. Kama vile Mungu, familia, shauku kwenye muziki na hata ubora. Namba tano inanikumbusha juu ya upendo na neema ya Mungu isiyo na mwisho juu ya maisha yangu kwamba yeye yuko pamoja nami kila wakati.
“Nilizaliwa mwezi wa tano na ninatoka katika familia iliyounganishwa na watu watano. Mama, baba, dada, kaka yangu na mimi mwenyewe kwa hiyo namba tano inawakilisha watu hawa ambao ni ulimwengu wangu,” anasema Abigail
Mbali na sauti nzuri ya uimbaji Abigail yuko vizuri katika upigaji wa vyombo mbalimbali vya muziki nayo anahusisha na namba tano.
“Nilijifunza kupiga ala ya muziki ya kwanza nilipokuwa na umri wa miaka mitano. Muziki tangu wakati huo umekuwa maisha yangu.
“Namba hii inawakilisha safari yangu ya muziki, na hadi sasa ninauwezo wa kupiga ala tano za muziki. Kwangu mimi, namba tano inawakilisha ubora wa kila kitu ninachofanya,” anasema Abigail.
Utakumbuka msanii huyo ana Extended Playlist (EP) moja aliyoipa jina namba tano. EP hiyo ilitoka mwaka 2023. Baada ya kuachiwa ilifanya vizuri hadi kutokea katika toleo la Apple Music, The Dotty Show.