Dar es Salaam. Kuanzia mwaka 2010 wasanii maarufu kutoka Marekani na Canada walikuja na mtindo wa kipekee katika nyimbo zao. Mtindo ambao ulifanya wakubalike na mashabiki kutoka sehemu mbalimbali za dunia.

Miaka hiyo wasanii wengi katika nyimbo zao walitupia kionjo cha mstari/kiitikio chenye maneno ‘Na Na Na Na’. Ngoma zilizofanya hivyo kwa asilimia kubwa zilifanya vizuri.

Haikuwa lazima kwa kila msanii kuweka mstari huo. Lakini ilikuwa kama mbinu ya kuvutia wasikilizaji, kwani maneno ya aina hiyo yalikuwa rahisi kuimba, kukariri huku yakiwafanya mashabiki waimbe wimbo mzima hata kama hawajui mistari mingine.

Mtindo huo ulianza kwa Rihanna kupitia wimbo wake akiwa na Drake wa ‘What’s My Name?’ ambapo sehemu ya ‘Na na na’ iligeuka kuwa kipande maarufu zaidi. Naye Akon aliufanya mstari huo kuwa sehemu kuu ya wimbo wake wa Right Now (Na Na Na), ambao ulimrudisha kwenye chati za dunia kwa kishindo.

Mtindo huo uliendelea kushika kasi kwa wasanii wengine. One Direction walifanikiwa kupata mashabiki wapya kupitia wimbo wa What Makes You Beautiful, huku Selena Gomez na Ariana Grande wakitumia mtindo huo kwenye nyimbo zao Come & Get It na Why Try. 

Kadri miaka ilivyokuwa ikisonga mbele, mtindo huu haukupotea. DJ Snake na Justin Bieber waliutumia tena kwenye wimbo wa Let Me Love You, huku Camila Cabello akiutumia kwenye wimbo wake wa Havana na kuufanya wimbo huo kuwa gumzo duniani kote. Aidha naye Trey Songz alienda mbali zaidi aliamua kuupa wimbo wake jina la ‘Na Na Na’ akionyesha nguvu ya mstari huo kwenye biashara ya muziki. 

Katika historia ya muziki inaelezwa kuwa hakuna mwanzilishi rasmi wa mtindo huo. Lakini kundi la muziki la The Beatles kupitia wimbo wao wa mwaka 1968, Hey Jude, ndio linatajwa kuufanya mtindo huo kujulikana na kutumika katika nyimbo mbalimbali za Pop.

Wadau wa muziki wametoa ushauri kwa mastaa wa sasa wakisema hit song si lazima kutumia maneno magumu na badala yake msanii anatakiwa kuangalia maneno rahisi ambayo shabiki anaweza kuyashika haraka ili kusaidia wimbo kujulikana zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *