Uingereza. Jina la Pedro Porro (26), si geni tena katika ulimwengu wa soka la kimataifa, beki huyo wa Tottenham Hotspur na timu ya taifa ya Hispania amejiweka kwenye ramani kutokana na bidii, nidhamu na kipaji chake kikubwa.
Hata hivyo, mbali na mafanikio yake uwanjani, maisha binafsi ya Porro yameanza kuvutia macho ya mashabiki wengi, hasa baada ya kuanzisha familia pamoja na mpenzi wake, Maria Hurtado.
Kwa muda mrefu, Porro amejipambanua kama mchezaji anayependa kuweka maisha yake ya faragha mbali na vyombo vya habari. Ila mapenzi, familia na baraka ya watoto vimefanya jina lake kuzungumzwa pia nje ya uwanja.
Ingawa hawajawahi kuweka wazi hadharani maelezo ya kina kuhusu siku ya kwanza walipokutana, vyanzo kutoka mitandao ya kijamii zinaonyesha kuwa uhusiano wao ulianza kwa utulivu na kwa msingi wa urafiki.
Chapisho lao la kwanza la pamoja kwenye Instagram lilionekana mwanzoni mwa 2024, likiwa ni picha ya kawaida iliyojaa tabasamu, ila mashabiki walitambua kuwa kulikuwa na kitu kikubwa zaidi ya urafiki.
Ingawa jina la Maria Hurtado halina umaarufu mkubwa katika vyombo vya habari, amejijengea picha kama mwanamke mtulivu, mwenye mapenzi ya dhati na anayempa Porro faraja kubwa maishani.
Kupitia machapisho yake mitandaoni, Maria amekuwa akionyesha wazi ni kwa kiasi gani anamuunga mkono Porro katika safari yake ya soka, akifuatilia mechi zake, mazoezi na nyakati muhimu za kazi yake.
“Nina bahati ya kukuona ukifanya kazi kila siku, kukuona ukipambana,” ni ujumbe wa Maria kwenda kwa Porro, akionyesha namna uhusiano wao ulivyo wa kuelewana pamoja na kuheshimiana.
Baada ya Porro kuhamia Tottenham Hotspur mnamo 2023, maisha yao yalihamia rasmi England, ikiwa ni mara ya kwanza kwa beki hiyo wa pembeni kucheza ligi kuu ya nchi hiyo maarufu kama EPL.
Huko wanafurahia maisha ya kawaida yasiyo na kelele nyingi, Maria mara nyingi huposti picha zinazoonyesha maisha ya nyumbani kwao, matembezi ya kawaida na nyakati za furaha wanazopitia kwa pamoja.
Kwa Porro, Maria amekuwa zaidi ya mpenzi amekuwa nguzo muhimu ya utulivu wa kihisia. Katika mahojiano mbalimbali, Porro amesisitiza umuhimu wa familia na watu wa karibu katika mafanikio yake.
Tunaweza kusema Porro kapenda boga na ua lake, hiyo ni kwa sababu kabla ya kupata mtoto wao wa pamoja, tayari Maria alikuwa na mtoto wa kike, Carla (2018) aliyempata katika uhusiano mwingine hapo wa awali.
Siku zote Carla amekuwa sehemu muhimu ya maisha ya Porro, ambaye amemkubali kama mtoto wake wa kambo na kumuonyesha upendo mkubwa bila kuingiza ubaguzi wowote katikati.
Kupitia picha na video wanazoposti, inaonekana wazi kuwa Porro ana uhusiano wa karibu sana na Carla. Kila mara wanacheza na kusafiri pamoja kama familia kwa ajili ya utalii au mapumziko.
Porro aliwahi kukiri katika mahojiano kuwa jukumu la kuwa baba si rahisi, hasa anapochanganya na ratiba ngumu ya soka la kulipwa. Hata hivyo, alisisitiza kuwa familia humpa nguvu na motisha zaidi ya kupambana.
Mnamo Machi 2, 2025, Porro na Maria walitangaza kuwa walikuwa wanatarajia kupata mtoto wao wa kwanza. Kupitia Instagram, walichapisha picha za hafla ya baby shower huku wakionekana wakiwa na furaha na matumaini.
“Tunakusubiri kwa mikono miwili iliyo wazi mwanangu. Mini Pedro Porro Jr,” Ujumbe huo ulithibitisha kuwa walikuwa wanatarajia mtoto wa kiume.
Furaha hiyo ilitimia rasmi Septemba 1, 2025, wakati mtoto wao wa kiume alipozaliwa. Mtoto huyo alipewa jina la Pedro, sawa na baba yake, ikiwa ni ishara ya urithi na upendo wa kifamilia.
Wazazi wote hawakusita kuonyesha furaha yao mitandaoni wakimtambulisha mtoto wao kwa mashabiki wao. Walitumia majina kama MiniPedro na Gordito, wakieleza kuwa mtoto huyo amegusa nyoyo zao.
“Karibu kwenye familia, mtoto mdogo. Utakua ukikuzwa kwa upendo na uangalizi mkubwa. Tunakupenda sana mwanangu,” alieleza Porro.
Ujumbe huo uliambatana na picha zilizogusa nyoyo za wengi, zikionesha familia hiyo ikifurahia baraka mpya. Walipokea pongezi kutoka kwa mashabiki na wachezaji wenzake wa zamani wa Sporting CP.
Ikumbukwe kuwa Porro alijiunga na Sporting msimu wa 2020/21 na aliitumikia klabu hiyo hadi 2022 kabla ya kuhamia Tottenham Hotspur. Akiwa na Sporting, alifunga mabao 12 na kutoa pasi za mabao 20 katika mechi 98.
Kwa sasa, Porro anaonekana si tu kama staa wa soka, bali pia kama mwanafamilia mwenye kujali na kuwajibika. Maisha yake na Maria yanaakisi hadithi ya mapenzi yenye uvumilivu, mshikamano na ukuaji wa pamoja.
Na kabla ya uhusiano wake na Maria, mnamo 2022, Porro aliwahi kuhusishwa na mwanamitindo Magui Corceiro ambaye aliwahi kuwa mpenzi wa mchezaji mwenzake, Joao Felix ila wote alikanusha uvumi huo.