
Rais wa zamani wa Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) amewataka watazamaji wa Kombe la Dunia wasisafiri kwenda Marekani kutokana na wasiwasi wa kiusalama.
Sepp Blatter, jana Jumatatu aliwaunga mkono mashabiki wa soka wanaotoa wito wa kususia Kombe la Dunia la mwaka huu nchini Marekani kwa sababu za kiusalama.
Kwa mujibu wa gazeti la Guardian, Blatter pia ameunga mkono kauli za Mark Pitt, wakili wa Uswisi wa kupambana na rushwa ambaye alifanya kazi na FIFA kuhusu mageuzi yanayowezekana wakati wa urais wa Blatter, akisema: “Mashabiki wanapaswa kukaa mbali na Marekani wakati wa mashindano ya Kombe la Dunia.”
Blatter ameongeza kwenye mitandao ya kijamii: “Nadhani Mark Pitt yuko sahihi kuhoji mashindano ya Kombe la Dunia huko Marekani.”
Inafaa kuzingatiwa kwamba Pitt ameyataja mauaji yaliyofanywa na afisa wa uhamiaji wa Marekani huko Minneapolis dhidi ya Renee Nicole Good, mama aliyekuwa na watoto watatu mapema mwezi huu huko Minneapolis, kama mojawapo ya sababu zinazowafanya mashabiki wasisafiri kwenda Marekani.
Uungaji mkono wa Blatter kwa maoni ya Pitt unafuatia mauaji ya raia mwingine wa Marekani, Alex Pratt, wikendi iliyopita ambaye pia alipigwa risasi na maafisa wa serikali ya Marekani.
Video iliyosambaa sana kwenye mitandao ya kijamii na kuthibitishwa na vyombo vya habari vya Marekani ilionyesha kuwa Pretti hakutoa silaha yoyote, na maafisa walimpiga risasi sekunde chache baada ya kummwagia usoni kemikali inayowasha na kumtupa chini.
Serikali ya Trump imekuwa ikikabiliwa na shinikizo linaloongezeka kuhusu msako wake mkali dhidi ya wahamiaji, hasa baada ya maafisa wa Shirikisho kumpiga risasi na kumuua Alex Pretti, muuguzi wa chumba cha wagonjwa mahututi aliyekuwa na umri wa miaka 37, siku ya Jumamosi, wakati wakijibizana naye kwenye barabara yenye barafu.
Marais wa zamani wa Marekani Barack Obama na Bill Clinton, wametoa wito kwa Wamarekani kusimama na kutetea maadili ya nchi yao baada ya mauaji ya pili ya raia mjini Minneapolis.