Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM) limetangaza kuwa watu wasiopungua 285 ni miongoni mwa wale waliolazimika kuyahama makazi yao kwenye kipindi cha siku mbili za karibuni katika miji ya Kadugli na Al-Kuwaik iliyoko kwenye Jimbo la Kordofan Kusini nchini Sudan kutokana na hali mbaya ya usalama.

Taarifa iliyotolewa IOM siku ya Alkhamisi imesema, maafisa wake wamethibitisha watu 85 wameondoka Kadugli, mji mkuu wa jimbo hilo, kutokana na hali mbaya ya usalama na operesheni ya kijeshi ya Januari 27 na 28.

Shirika hilo la UN limeongeza kuwa watu wengine 200 waliondoka katika makazi yao siku ya Jumatano katika eneo la mji wa Al-Kuwaik sehemu ya mashariki huko Kordofan Kusini, ikitajwa pia sababu ya kuvurugika hali ya usalama kama chanzo cha kuondoka kwao.

Kwa mujibu wa IOM, familia hizo zilielekea katika jimbo la White Nile kusini mwa Sudan na eneo la Kelik katika jimbo jirani la Kordofan Magharibi.

Shirika hilo la UN limetahadharisha kuwa hali katika eneo hilo ingali “ni tete,” likieleza kwamba lingali linafuatilia kwa makini kinachoendelea.

Mapema wiki hii, IOM ilitangaza kuwa idadi ya waliohama makazi yao eneo la Kordofan imeongezeka hadi kufikia watu 88,316 katika kipindi cha zaidi ya miezi miwili kutokana na vita vinavyoendelea kati ya Jeshi (SAF) na wapiganaji wa Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF).

Tangu Aprili 15, 2023, Jeshi la Sudan na RSF zimekuwa zikipambana katika vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo wapatanishi wa kanda na kimataifa wameshindwa kuvihitimisha hadi sasa. Vita hivyo vimesababisha vifo vya maelfu ya watu huku mamilioni ya wengine wakilazimika kuyahama makazi yao…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *