Uamuzi wa shirika la Uhamiaji na Forodha la Marekani (ICE) wa kukataa kutoa ruhusa ya muda ya sababu za kibinadamu kwa mzazi aliyeko kizuizini kuhudhuria mazishi ya mwanawe kimelaaniwa vikali na watumiaji wa mitandao ya kijamii huku baadhi yao wakiuelezea uamuzi huo kuwa ni “mchafu na wa kinyama”.

Maher Tarabishi, mkazi wa Arlington, Texas mwenye umri wa miaka 62, mwenye asili ya Jordan, amekuwa akishikiliwa katika Kituo cha Magereza cha Bluebonnet huko Anson, Texas, tangu alipokamatwa na maajenti wa ICE mnamo Oktoba 28. Mwanawe, Wael, mwenye umri wa miaka 30, alifariki mnamo Januari 23 kutokana na matatizo yanayohusiana na ugonjwa wa Pompe, moja ya maradhi adimu ya kijenetiki.

Wael alikuwa raia wa Marekani, na baba yake alikuwa akimhudumia kimatunzo kama mlezi wake mkuu kwa miongo kadhaa.

Maafisa wa ICE walikataa ombi la Maher la kuhudhuria mazishi ya Wael, yaliyopangwa kufanyika jana Alkhamisi, kitendo ambacho kimelaaniwa na kuibua malalamiko mengi mitandaoni.

Ali Elhorr, wakili anayemwakilisha Maher, alilithibitishia jarida la People kwamba ICE ilikataa ombi hilo siku ya Jumanne. Shirika hilo halijaelezea hadharani kwa nini njia mbadala kama vile kuhudhuria kwa kusindikizwa au kuachiliwa kwa muda mfupi hazikuidhinishwa.

Wael aligunduliwa kuwa na ugonjwa wa Pompe alipokuwa na umri wa miaka minne. Ni hali ambayo hudhoofisha misuli hatua kwa hatua na inaweza kusababisha matatizo yanayohatarisha maisha. Kwa mujibu wa familia yake, Maher alihusika sana katika masuala yote ya matunzo ya mwanawe.

Mnamo Novemba 20, Wael alilazwa hospitalini kabla ya kufariki dunia siku ya Ijumaa iliyopita…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *