Serikali imeipongeza Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa mchango wake mkubwa katika sekta ya madini nchini, ikitaja miongoni mwa mambo mengine dhamira yake katika uchimbaji madini unaowajibika, ulipaji kodi, utoaji wa ajira na kushiriki katika maendeleo ya jamii katika kipindi cha miaka 25 ya uendeshaji wake nchini.

Akizungumza katika hafla ya chakula cha jioni ya maadhimisho ya miaka 25 ya GGML Jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, amesema rekodi ya utendaji ya GGML inaonesha wazi namna uchimbaji madini unaowajibika unavyoweza kuunga mkono vipaumbele vya maendeleo ya taifa.

Ameongeza kuwa mchango wa GGML kupitia ulipaji kodi, uanzishaji wa ajira na utekelezaji wa miradi ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) umeimarisha sekta ya madini pamoja na uchumi mpana wa Taifa.

Hafla hiyo imewakutanisha viongozi wakuu wa Serikali, Wakurugenzi Wakuu wa taasisi mbalimbali, Wakurugenzi Watendaji, wanadiplomasia pamoja na wadau muhimu wa sekta binafsi.

Maadhimisho hayo yalipambwa na jukwaa la simulizi lijulikanalo kama Stori za Dhahabu, lililobuniwa kukusanya na kuhifadhi uzoefu wa watu ambao maisha na shughuli zao zimeguswa na uwepo wa GGML tangu kuanza kwa shughuli zake mwaka 2000.

Jukwaa hilo linaangazia simulizi kutoka kwa wafanyakazi waliodumu kwa muda mrefu, wakandarasi na wanufaika wa miradi ya maendeleo ya jamii inayoungwa mkono na GGML.

Kama sehemu ya maadhimisho, GGML ilizindua filamu ya ‘Stori za Dhahabu’, inayoelezea safari ya mgodi huo kwa kipindi cha miaka 25 na kuonesha simulizi zinazohusu mgodi huo.

Hafla hiyo imehitimishwa kwa tafakari juu ya umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, wakandarasi na jamii katika safari hiyo ya GGML kwa kipindi cha miaka 25.

Maadhimisho ya Stori za Dhahabu yameiweka kumbukumbu hiyo ya miaka 25 kama tukio la kukumbukwa linaloonesha umuhimu wa uwekezaji wa GGML katika sekta ya madini nchini Tanzania.

#StarTvUpdate

(Feed generated with FetchRSS)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *