Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, amesema awamu inayofuata ya mazungumzo ya amani miongoni mwa maafisa waandamizi kutoka nchi hiyo, Urusi na Marekani itafanyika mjini Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu, UAE mnamo Februari 4 na 5.
Nchi hizo tatu zilifanya mazungumzo ya kwanza ya amani ya ngazi ya juu mnamo Januari 23 na 24, katika mji huo mkuu wa UAE.
Zelenskyy amebainisha ratiba hiyo ya awamu ya pili ya mazungumzo ya pande tatu katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii Februari mosi.
Zelenskyy aliandika, “Ukraine iko tayari kwa mazungumzo ya kweli.” Aliongeza kuwa “Tuna nia ya kuhakikisha kwamba matokeo yanatuleta karibu na mwisho halisi na wa heshima, wa vita hivi.”
Inaaminika kuwa Ukraine na Urusi bado zinatofautiana sana kuhusu suala la eneo. Urusi inatoa wito kwa wanajeshi wa Ukraine kuondoka kutoka eneo la mashariki la Donbas, matakwa ambayo Ukraine inaona ni vigumu kukubali.
Urusi ilitangaza kwa upande mmoja kuichukua Donbas na maeneo mengine mawili ya Ukraine mnamo Septemba 2022, miezi michache tu baada ya kuanza uvamizi wa nchi hiyo mnamo Februari mwaka huo.
Wakati huo huo, maafisa wa hali ya hewa wa Ukraine wanatarajia halijoto ya chini ya usiku kucha huko Kyiv kushuka hadi karibu nyuzi 24 hasi za Selisiasi mpaka Februari 4. Pia wanatabiri kwamba halijoto ya juu ya mchana katika eneo hilo itafika karibu nyuzi 12 hasi tu katika kipindi hicho hicho.
Utabiri huu unakuja wakati ambapo mashambulizi ya kijeshi ya Urusi dhidi ya miundombinu ya nishati ya Ukraine yakiwazuia watu kupata umeme na kupashajoto kote nchini humo.