Rais Masoud Pezeshkian ameagiza kuanza upya kwa mazungumzo kati ya Iran na Marekani kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran.

Ripoti ya Press TV imebaini kuwa ,vyanzo vinavyofahamu suala hilo viliambia mashirika ya habari ya Fars na Tasnim kwamba Rais Pezeshkian Jumatatu alitoa ruhusa rasmi kwa mazungumzo hayo kuanza upya.

Hata hivyo, muda na eneo la mazungumzo hayo havikutajwa mara moja.

Mazungumzo kati ya Tehran na Washington, yaliyokuwa yakiratibiwa na Oman, yalivunjika Juni mwaka jana baada ya Marekani kujiunga na utawala wa Israel katika mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran, yaliyojumuisha mashambulizi kwenye vituo vya nyuklia vya Iran.

Wakati huohuo, shirika la habari la ISNA liliripoti kuwa ujumbe wa Iran na ule wa Marekani unatarajiwa kukutana kwa mazungumzo ndani ya siku chache zijazo.

Kama ilivyokuwa katika awamu zilizopita, mazungumzo yanayoweza kufanyika yataongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, na mjumbe mwandamizi wa Rais wa Marekani Donald Trump, Steve Witkoff. 

Kwa mujibu wa vyanzo kadhaa, kufuatia safari ya Araghchi nchini Uturuki Ijumaa na juhudi za Ankara kuandaa mazungumzo kati ya Tehran na Washington, mazungumzo hayo yanaweza kufanyika nchini Uturuki, yakihusisha pia Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan.

Mbali na Uturuki, Qatar na Misri pia zimefanya juhudi za kidiplomasia kuandaa mazungumzo hayo, kama sehemu ya jitihada za kuzuia Marekani kuanzisha vita vingine vya kichokozi dhidi ya Iran.

Maafisa wa Iran wamesisitiza wazi kuwa shambulio lolote kutoka Marekani au Israel litakabiliwa na majibu ya haraka na makali, na linaweza kusababisha vita kuenea eneo lote la Asia Magharibi.

Akizungumza katika mahojiano na CNN Jumapili, waziri wa mambo ya nje wa Iran alisema Marekani inapaswa kutumia fursa iliyopo kufikia makubaliano  Tehran kwa msingi wa haki, akionya kuwa uchokozi wowote wa kijeshi utapelekea eneo zima likumbwe na “janga.”

Mwishoni mwa wiki Marekani ilionyesha hamu ya kufanya mazungumzo na Iran. Akizungumza na waandishi wa habari ndani ya ndege ya Air Force One Jumamosi, Rais wa Marekani Donald Trump aliashiria kuwa Marekani inataka kufanya mazungumzo na Iran.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *