Dar es Salaam. Mwigizaji wa muda mrefu huko Hollywood, Angelina Jolie, (50) hajawa katika uhusiano wa kimapenzi tangu alipokamilisha talaka yake na aliyekuwa mume wake, Brad Pitt, (62), mnamo Desemba 2024.

Wawili hao waliofunga ndoa mwaka 2014, kwa mara ya kwanza kuonekana pamoja hadharani na kuthibitisha uhusiano wao ilikuwa 2005, muda mfupi baada ya Brad kutengana na aliyekuwa mkewe, Jennifer Aniston.

Kwa mujibu wa chanzo cha karibu kilichozungumza na Jarida la People, kimedokeza kuwa mwigizaji huyo kwa sasa ameweka kipaumbele katika malezi ya watoto wake pamoja na kazi yake ya uigizaji.

“Amekuwa na shughuli nyingi sana kwa miaka ya hivi karibuni, hivyo kuweka miadi ya kimapenzi halijawa jambo la muhimu kwake. Bado hajawa na mpenzi mpya,” chanzo hicho kilisema.

“Kwa kiasi kikubwa amejikita katika malezi ya watoto wake akiwa kama mlezi pekee tangu talaka, hivyo hapo ndipo ameelekeza nguvu zake nyingi,” imeelezwa.

Ikumbukwe Angelina na Brad ni wazazi wa watoto sita; Maddox (24), Pax (22), Zahara (21), Shiloh (19), na mapacha Knox na Vivienne wenye miaka 17. Watoto watatu wakubwa wamewasili, na watoto wa mwisho ndio waliowazaa.

“Siku zote amekuwa akipenda sana kuwa mama bora, hivyo anataka kuhakikisha kila mtoto anafanikiwa na anaonekana kuwa katika hali nzuri ya kimaisha,” chanzo hicho kinaongeza.

Katika filamu yake mpya, Couture (2025), Angelina ameigiza kama mtengenezaji filamu anayepitia kipindi cha talaka huku pia akigundulika kuwa na ugonjwa wa saratani ya matiti.

Akizungumza na Time France mnamo Desemba mwaka uliopita, alisema filamu hiyo imebeba hadithi yake binafsi. Kwa mara ya kwanza Couture ilioneshwa katika Tamasha la Filamu la Kimataifa la Toronto (TIFF) 2025 hapo Septemba.

Ikumbukwe kuwa mama yake Angelina, Marcheline Bertrand, alifariki mwaka 2007 akiwa na umri wa miaka 56 kutokana na saratani ya matiti na ovari.

Mwaka 2013, Angelina alifanyiwa upasuaji wa kuondoa matiti yake yote mawili ikiwa ni sehemu ya kinga baada ya vipimo kuonesha kuwa alikuwa na hatari kubwa ya kupata saratani.

Hapo awali, chanzo kingine kiliiambia People kuwa nyumba ya Angelina iliyopo Los Angeles ilikuwa katika mnada baada ya kufanyiwa ukarabati.

Chanzo hicho kilisema kuwa mwigizaji huyo hakuwahi kutaka kuishi Los Angeles kwa muda mrefu lakini alilazimika kufanya hivyo kutokana na makubaliano ya malezi kati yake na mzazi mwenziye.

Angelina ambaye ataonekana pia katika filamu ya Anxious People, taarifa za ndani zaidi zilidai ana mpango wa kuhama mara tu watoto wake mapacha, Knox na Vivienne watakapofikisha umri wa miaka 18 hapo Julai 12, 2026.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *