Dar es Salaam. Siyo suala la kushangaza msanii aliyesajiliwa katika rekodi lebo  fulani kuacha lawama pindi anapotengengana na lebo husika. Lawama hizi huweza kuwa na ukweli na nyingine kuongezwa chumvi.

Hii siyo Tanzania tu. Hilo ni tatizo la kidunia katka sekta ya muziki. Baada ya kutokea kwa matukio hayo. Hatimaye imefika zamu ya Macvoice aliyekuwa msanii wa Next Level Music (NLM) inayomilikiwa na Rayvanny. 

Msanii huyo aliyesajiliwa NLM mwaka 2021 mapema wiki hii akiwa kwenye moja ya mahojiano alidai  hakuwahi kupokea kiasi chochote cha pesa kutoka kwenye lebo iliyokuwa ikimsimamia, hadi kufikia hatua ya kukosa pakulala.

Jambo lililoibua hisia mbalimbali kutoka kwa wadai mbalimbali wa muziki. Hakuishia hapo alidai ili kujitoa katika lebo hiyo alitakiwa kulipa Sh100 bilioni. Kiasi cha pesa ambacho hakikuwa kwenye mkataba wake, kwani mkataba ulimtaka alipe Sh1 Bilioni tu. Leo hatujadili mwenye matatizo nani

Tukio hili linakumbusha kilichotokea kwa baadhi ya wasanii kama lile la  Harmonize alipotakiwa kulipa faini ya Sh 600 milioni alipotaka kujitoa WCB rekodi lebo iliyomtoa mwaka 2015 kabla ya kutambulishwa kwa Rayvanny mwaka uliofuata.

Baada ya kujitoa WCB  Harmonize alianzisha lebo yake ya Konde Gang, kisha akamsajili Ibraah na baadaye akaongeza wasanii wengine akiwemo Country Boy pamoja na kuwavuta wasanii waliokuwa wanafanya kazi Kings Record ya Alikiba, Cheedy na Killy.

Baada ya kufanya kazi kwa kipindi kirefu naye Ibraah yalimkuta alipotaka kijitoa Konde Gang alidai lebo hiyo ilimtaka alipe Sh1 bilioni.

Hakika huu ni mwiba unaoendelea kuwachoma wamiliki na wasanii waliopo kwenye lebo za muziki. Hivyo basi unahitaji utatuzi kama wanavyotoa mbinu wadau mbalimbali wa muziki.

Mambo kumi ya kuzingatia 

Mtayarishaji nguli wa muziki nchini Bob Manecky amefafanua vitu kumi vya kuzingatia kabla ya msanii kusaini mkataba.

Amesema kwanza ni umiliki wa kazi (Masters & Publishing) Masters, nani anamiliki rekodi zako?

“Bora wewe ubaki mmiliki au iwe license ya muda. Publishing (uandishi wa nyimbo), hakikisha haki za uandishi hazichukuliwi bila ridhaa yako. Pili ni mgawanyo wa mapato (Royalties), angalia asilimia ya streaming & downloads YouTube, Content ID

“Shows na performances. Uliza unalipwa lini? (kila miezi mingapi) na kwa njia gani?Tatu muda wa mkataba epuka mikataba ya miaka mingi bila uhakika “Album nyingi” bila njia ya kutoka. Tafuta kipengele cha termination / exit clause.

“Nne udhibiti wa ubunifu (Creative Control) nani anaamua style ya muziki? Artwork & branding? Collabo unazofanya? Usikubali kubanwa sana kama msanii.

“Tano gharama na Madeni (Recoupment) Promo, video, studio ni nani analipa? Kama ni lebo inalipa, je gharama zinakatwa kwenye mapato yako kabla hujalipwa? Elewa deni kabla ya kusaini. 

“Sita Promotion na majukumu ya Lebo, je, lebo imeandika wazi itafanya nini? Marketing Radio/playlist pitching, PR na distribution. Epuka ahadi za mdomo ziwe kwenye mkataba

“Saba mkataba ni ndani ya nchi? Africa? Dunia nzima? World deal bila nguvu ya promotion ni hatari. Nane brand deals  na live shows lebo inachukua asilimia ya shows? endorsements? Kama ndiyo, asilimia iwe wazi na ya haki.

“Tisa accounting na transparency, hakikisha una haki ya kupata taarifa za mapato (statements). Kufanya audit kama kuna mashaka. 

“Kumi msaada wa kisheria usisaini peke yako. Pata mwanasheria wa burudani AU, mtu mwenye uzoefu wa mikataba ya muziki,”ameeleza Bob Manecky

Hata hivyo, akizungumza na  Mwananchi Mkuu wa Kitengo cha Sheria Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Christopher Kamugisha amesema janga hilo limekuwa kubwa kwa sababu wasanii wachache tu ndiyo wanaofika Basata kupewa msaada wa kisheria kabla ya kusaini mikataba.

“Kwa mujibu wa kanuni zetu zinasema  kabla mtu hajasaini mkataba  wowote, anaweza akaleta ukapitiwa na anashauriwa. Wasanii tunawashauri mara kwa mara wawasilishe  nakala ambayo wanaletewa na lebo, msanii au hata na meneja.

“Tunatapitia tunamshauri,  lakini mkataba ni makubaliano wa pande mbili kila mtu. Kinachofanyika ni wachache wanaleta wengine wanaleta wakiwa wamepata shida baada ya kusaini,”anasema.

Utakumbuka Mei 6 2025, Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) lilitangaza kuwa lipo mbioni kuanzisha muundo wa mikataba ya kazi za muziki, ambao unalenga kupunguza changamoto zinazoikumba sekta hiyo nchini.

Mikataba hiyo ya mfano itakuwa mwongozo kwa wasanii, mameneja wao na kampuni za kurekodi (record labels), kuhusu mambo muhimu ya kuzingatia ili kusaidia kupunguza matatizo ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara katika tasnia ya muziki.

“Kumekuwa na changamoto kubwa sana linapokuja suala la mikataba. Sisi kama Baraza la Sanaa tumegundua kuwa mivutano mingi tunayopokea inatokana na mikataba isiyoeleweka vizuri.

“Kwa hiyo, tunakwenda sasa kama Baraza kuwa na model ya mikataba, ambayo hata kama haitakuwa kamili kwa asilimia mia moja, angalau itasaidia kupitia maeneo muhimu ili kuondoa changamoto ambazo tumeziona.,” alisema Afisa Sanaa Mwandamizi kutoka BASATA, Abel Ndaga.

Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) Dk. Herbert Makoye, akitoa suluhu la tatizo hilo  amesema wasanii wawe na tabia ya kusoma na kuielewa mikataba kabla ya kusaini ili kuepusha uadui wakati wanataka kujitoa kwenye lebo hizo.

“Kuna kitu kinaitwa mihemko, kama mtu kahangaika zaidi ya miaka mitano barabarani,  hamadi unapata kazi unasaini haraka asije akasaini mwingine. Baadaye ukijitambua unagundua ulisaini vitu ambavyo siyo.

“Inawezekana kuna wengine wanaingia kwenye lebo bila mikataba, alafu ndiyo inafuata baadaye. Pamoja na hayo lebo  nazo zisiwawekee wasanii masharti magumu. Zikumbuke hazipo tu kwa ajili ya biashara kutafuta hela  bali ni pamoja na kukuza tasnia ya muziki. Ili mtu akitaka kuondoka asiwe adui,”amesema.

Amesema  msanii akifikia hatua ya kuingia kwenye lebo aangalie mikataba  na siyo lazima aijue yeye  tu badala yake  atumie wanasheria.

“Wapeleke kwa wanasheria na hapa Tanzania tumesema hivi ukipata mkataba nenda  Basata kuna mwanasheria wa bure hana haja ya kufanya siri. Mwanasheria anatafsiri vyote maana mkataba unasaini baada ya  majadiliano unaweza kuomba hata kuondoka nao,”amesema. 

Msanii wa muziki wa Singeli nchini, Menja Kunta amesema kuna umuhimu wa wasanii  kuelimishwa kabla ya kuingia kwenye lebo. 

“Binafsi nimekaa kwenye lebo zaidi ya moja nafikiri inabidi wasanii waandaliwe kisaikolojia. Kwa sababu wanapochukua msanii anakuwa hana chohote kila anacholetewa kwenye maisha yake kinakuwa kipya msanii hajawahi kuwa na gari anapewa, anakaa nyumba nzuri.

“Kila kitu anapewa kama mimi nilitolewa Temeke nikapangiwa Ununio mwaka 2018 kwa hiyo nikaanza kuishi maisha mazuri. Menejimenti zetu zinawekeza sana. Lakini kabla ya kuwachukue wasanii muwe mnawapa mwongozo kwamba ni biashara ili kupunguza hizi lawama za kila siku,”amesema.

Naye msanii wa muziki wa Hip Hop, Musa Mabumo maarufu kama Bando, amesema kuwepo kwa muundo sawa ya  mikataba kutoka Basata kutapunguza migogoro nchini kwenye sekta ya burudani.

“Nadhani model  zitazotolewa na Basata ziwe za pande mbili zimwangalie msanii na pia mwekezaji anayemuunga mkono. Ziwe na usawa ili isionekane msanii pekee ndiye anayestahili huruma, bali hata mwekezaji apewe haki yake. Hilo litaongeza imani na kuvutia wawekezaji zaidi kwa wasanii,” alisema Bando.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *