Israel imetangaza mapema Jumatatu asubuhi, Machi 9, kwamba imefanya mashambulio mapya nchini Iran dhidi ya “miundombinu ya utawala” na huko Beirut, Lebanon, dhidi ya malengo ya Hezbollah. Iran inaendelea kulipiza kisasi kwa mashambulizi katika eneo la Ghuba.

Imechapishwa:

Dakika 2 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Israel imebaini leo Jumatatu asubuhi kwamba imeanzisha wimbi la mashambulio dhidi ya “miundombinu ya utawala wa kigaidi wa Iran” katikati mwa Iran. Hili ni shambulizi la kwanza kama hilo tangu kutangazwa kwa uchaguzi wa Kiongozi Mkuu mpya, Mojtaba Khamenei. Mashambulizi ya Israel pia yamelenga miundombinu ya Hezbollah huko Beirut, ambapo milipuko imesikika.

Iran inaendelea kulipiza kisasi kwa mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya Israel na mataifa ya Ghuba. Siku ya Jumatatu asubuhi huko Bahrain, shambulio la ndege zisizo na rubani za Iran liliwajeruhi raia 32, wanne kati yao wakiwa wamejeruhiwa vibaya, katika kisiwa cha Sitra, kulingana na Wizara ya Afya, kama ilivyoripotiwa na Shirika la Habari la Bahrain. Iran pia ilirusha makombora yake ya kwanza kuelekea Israel siku ya Jumapili kufuatia kuchaguliwa kwa Kiongozi Mkuu mpya wa Iran.

Mapigano makali ya ardhini yalifanyika usiku wa Jumapili kuamkia Jumatatu kati ya Hezbollah na jeshi la Israel mashariki mwa Lebanon. Kundi hili la Kishia limesema kwamba linapambana na vikosi vya Israel vilivyotua kwa helikopta mashariki mwa Lebanon kutoka mpaka wa Syria. Hezbollah imeongeza kuwa wanajeshi wa Israel walifika kwa “helikopta zipatazo 15” muda mfupi baada ya saa 10 alfajiri.

Kulingana na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa, angalau watu 1,332 wameuawa nchini Iran tangu kuanza kwa uhasama, wakiwemo wasichana wa shule 175 na wafanyakazi wa shule katika shambulio dhidi ya shule ya wasichana huko Minab, kusini mwa nchi. Idadi hii, ambayo haikuweza kuthibitishwa, huenda haijumuishi majeruhi wa kijeshi wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Nchini Lebanon, mashambulizi ya Israel yamewaua watu wasiopungua 394 tangu mzozo huo ulipoenea nchini humo siku ya Jumatatu.

Siku ya Jumapili jioni, Baraza la Wataalamu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lilimteua mtoto wa Ali Khamenei, Mojtaba Khamenei, kuwa Kiongozi Mkuu mpya. Wakati huo huo mapigano ya ardhini kati ya Hezbollah na wanajeshi wa Israel waliotua kwa helikopta yalikuwa yakiendelea mashariki mwa Lebanon usiku wa Jumapili kuamkia Jumatatu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *