Safari ya Rosa Ree inavyoshindwa kujitenga na NavyKenzoSafari ya Rosa Ree inavyoshindwa kujitenga na NavyKenzo

Dar es Salaam. Wamepita  wasanii wengi wa kike wanaochana na kuitingisha tasnia ya Bongo Fleva. Kina Zay B, Sister P, Raha P, Stella mwangi, Chemical, Stosh, Pinky, Tammy the Baddest, Cindy Rulz, Frida Amani na Rosa Ree na wengine.

Huu ni ujasiri. Kuchana ‘kurap’ mbele ya wanaume na kufikisha ujumbe si kazi rahisi. Hii ni kwa sababu miaka ya nyuma aina hii ya muziki ilihusishwa zaidi na upande mmoja ‘wanaume’ ukaonekana wa kihuni na hivyo kwa mwanamke kujihusisha nao jamii ingemtenga kama siyo kumwona amepotoka.

Hata hivyo, kwa ujasiri huu ndiyo hapo majina yakaibuka wanawake wakishindana kuchana kwenye vipaza sauti na kuingia studio akiwamo mmoja wa marapa wakali kwa sasa nchini Rosa Ree.

CHANGAMOTO ZAMWINGIZA STUDIO

Majina yake kamili ni Rosary Robert Iwole na alizaliwa Arusha na kusomea Kenya alikomaliza elimu ya msingi.

Baada ya kupitia changamoto nyingi katika maisha, alizibadilisha na kuwa dili akizitungia mistari na kuamua kuingia studio kwa mara ya kwanza mwaka 2015 na The Industry Studio ndio ilikuwa ya kwanza kufanya nayo kazi akitoa nyimbo kama ‘One Time’, ‘Asante Baba’, ‘Kupoa’,  na nyingine zilizombeba. Hapa anakumbuka alivyoanza kazi zake na alivyoondoka katika studio hiyo.

“NavyKenzo wamekuwa na mchango mkubwa kwenye karia yangu kuniamini, siyo kazi rahisi,” anasema na kuongeza aliamua kufanya muziki wa Hip Hop ili kuonyesha hata wanawake wanaweza kumudu presha ya kazi hiyo lakini bila kubadili mwonekano wake kisa kuna ushindani na wanaume.

HAIKUWA RAHISI

Ni ngumu kwa wanawake kushindana na majina kama Profesa Jay, Mr Blue, marehemu Albert Mangwair (enzi zake), Fid Q, Juma Nature, Inspactor Harun, AY, Mwana FA na wengine wengi.

Ambacho kingewapa nguvu wanawake ilikuwa ni kushirikisha wanaume katika ngoma zao na ni wachache sana waliimba wenyewe ngoma zote.

Hata hivyo, kwa Rosa Ree amekuwa jasiri na kumshirikisha msanii wa kiume ni kuamua mwenyewe lakini ana uwezo wa kusimama mwenyewe na ngoma zikahit na anasema kimwonekano hawezi kubadilika kisa aina ya muziki anaofanya.

“Ili utoboe unatakiwa uwe mzito na uwe unavaa kidume nikakataa hilo, staili yangu iko hivi kujiweka mwanamke lakini siwezi kuigiza kama mwanamume hilo halikunibadilisha.”

Amewadhihirishia mashabiki na wadau wa sanaa uwezo haupimwi kwa jinsia bali kipaji na kuthubutu na ndo hapo alipoachia ngoma mfululizo zilizotamba kama Dip n Whine It (2019), Kanairo (2023), Mama Omollo (2023), Watatubu (2023) na nyingine nyingi zilizompa umaarufu mkubwa ikiwamo uliomtambulisha wa ‘One Time’.

“’One Time’ ilikuwa ngoma kali kwa sababu nilitaka kuwaaminisha watu naweza niliambiwa wewe ni mwanamke na huwezi unatakiwa kufanya muziki wa aina hii,” anasema na kuongeza, aliambiwa sana aimbe kjwa sababu yeye ni mwanamke lakini kuonyesha anaweza ndiyo maana akawaonyesha kutokana na kazi zake.

HAAMINI KATIKA MISINGI YA HIP HOP

Anasema kazi ya muziki hasa Hip Hop ni kusema ukweli na hilo amekuwa akilitekeleza kwa kutumia misingi na utamuduni wa muziki huo.

Hata hivyo, hajifungi katika misingi hiyo kwani kuna mingine haiendani na mwonekano wa mwanamke na anapingana nayo.

“Misingi ni mizuri kwa sababu ndiyo inatuonyesha njia. Kama mwanamume unatakiwa uvae hivi, unyoe hivi au ufanye hivi. Kama mwanamke unatakiwa ukae hivi, uvae hivi upendeze wewe ni ua unatakiwa unukie.

“Mimi sio muumini wa kuzingatia misingi na nafanya kile ninachokitaka. Sina mipaka na kazi zangu,” anasema na kusisitiza siyo lazima mwanamke awe na mwonekano wa mwanamume ndiyo awe msanii, hata ukijiweka kama ulivyo, watu watakusikiliza tu.

HAKATI TAMAA, HAPOI

Anasema anapenda kuwahamasisha wanawake katika nafasi mbalimbali kwa kuonyesha wanaweza na si kukaa tu na kudharaulika.

“Napenda kuwahamasisha wanawake sio tu kwenye muziki, bali hata maeneo mengine, iwe sanaa, biashara na mambo mengine. Kuna mtu aliniambia nina hadhi ya kufanya kazi ofisini, lakini nikaona huko siwezi jao mwonekano niliambiwa hivyo. Mungu wetu hachagui na sikutaka kuambiwa cha kufanya. Muziki upo kwenye damu na familia yangu inanisapoti. Niliamua kuacha kazi na kurudi kwenye muziki.”

Anasema kutokana na muziki, mwanzo alipoacha kazi ya ofisini na kufanya muziki, alikuwa anakosa hata hela ya matumizi lakini alikomaa na kuanza kushika pesa na amekuwa akifanya shoo nyingi na aliwahi kupata hadi Dola 12,000 sawa na zaidi ya Sh30 milioni na alipewa yote.

“Hakukuwa na mtu kati, nililipwa zote na nashukuru kazi yangu ililipa,” anasema na kuwataka Watanzania  hasa wanawake wathamini sana sanaa kwani ni ajira na inalipa kwa kuonyesha juhudi kama kazi nyingine.

Tofauti na dhana wasanii wa kike lazima wategemee kubebwa au skendo ili wabaki juu, Rosa Ree alichagua kujenga brand ya msichana mkali.

“Hakuna kitu muhimu kama kuwa wewe katika kitu chochote, mimi kuwa mimi inanitofautisha na wasanii wengine sio kwenye rap hadi kwenye muziki wa Bongo Fleva,” anasema.

TUZO ZAMFUATA

Miongoni mwa tuzo alizowahi kuzinyakua mwanadada huyo ni East Africa Arts & Entertainment Awards (EAEA) kama Msanii Bora wa Kike wa Hip Hop 2022, mwaka 2023 alichukua tuzo mbili za Muziki Tanzania (TMA) kama msanii Bora wa Kike wa Hiphop na wimbo Bora wa Hip Hop Blueprint.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *